Wizara Ya Afya

CHUO CHA AFYA RUFIJI KUONGEZA WATAALAMU NA KUBORESHA UTOAJI HUDUMA ZA AFYA

Posted on: October 4th, 2026

Na Clement Robert WAF, Pwani - Rufiji

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema ujenzi wa Chuo cha Afya Samia Suluhu Hassan pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ni hatua kubwa itakayosaidia kuongeza wataalamu wa afya na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani na maeneo jirani.

Ameyasema hayo leo Oktoba 04, 2026, mkoani Pwani, Wilaya ya Rufiji wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Chuo cha Afya cha Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Mchengerwa amesema chuo hicho kitakuwa na nafasi muhimu katika kuzalisha wataalamu wa afya, hususan katika kada zinazohitajika, na hivyo kusaidia kukabiliana na upungufu wa wataalamu unaoikabili sekta ya afya katika maeneo mbalimbali.

Amesema uwepo wa chuo hicho pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kutasaidia wananchi wa Rufiji, Kibaha, Kisarawe, Mafia, Mkuranga na maeneo mengine ya jirani kupata huduma bora za afya karibu na maeneo yao, huku wanafunzi wa kada mbalimbali za afya wakipata eneo la kujifunzia na kufanya mafunzo kwa vitendo.

“Jengo bila wataalamu halitoshi. Ndiyo maana Serikali imeamua kujenga chuo pamoja na hospitali, ili wataalamu hawa waweze kuzalishwa na kusaidia kumaliza changamoto zilizopo katika maeneo yetu,” amesema Mhe. Mchengerwa

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema maendeleo yanayoendelea katika Mkoa wa Pwani, hususan Rufiji, yanaonesha namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyowekeza katika maendeleo ya wananchi. Amesema Rufiji ya sasa si Rufiji ya zamani kutokana na miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa katika eneo hilo.

Ametaja uwepo wa miradi mikubwa ya kitaifa katika Bonde la Mto Rufiji, ikiwemo uzalishaji wa umeme, pamoja na fursa kubwa za uwekezaji, kilimo na viwanda, kuwa ni miongoni mwa mambo yanayobadilisha sura ya eneo hilo na kuongeza fursa kwa wananchi.

Mhe. Mchengerwa amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Pwani kwa juhudi za kuhamasisha uwekezaji na kusimamia fursa mbalimbali za maendeleo katika mkoa huo, akisema uwekezaji huo utasaidia kuongeza ajira na kuchochea uchumi wa wananchi.