Wizara Ya Afya

BONANZA LA 360 KUWAFIKIA VIJANA ZAIDI YA 3,000 MWANZA, KUTOA ELIMU NA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: October 29th, 2026

Na Atley Kuni, WAF-Mwanza

Bonanza la 360 linaloratibiwa na Wizara ya Afya linatarajia kuwafikia zaidi ya vijana 3,000 mkoani Mwanza, likilenga kutoa elimu na huduma mbalimbali za afya, hususan afya ya uzazi kwa vijana. Bonanza hilo linafanyika kwa siku tatu, kuanzia Oktoba 29 hadi 31, 2026, katika Chuo cha Ualimu Butimba, jijini Mwanza.

Akizungumza leo, Oktoba 29, 2026 jijini Mwanza, wakati wa maandalizi ya bonanza hilo, Mratibu wa Afya ya Uzazi kwa Vijana kutoka Wizara ya Afya, Bw. Gerald Kihwele, amesema bonanza hilo litatoa fursa kwa vijana kupata elimu kuhusu afya ya uzazi, lishe bora, UKIMWI, umuhimu wa kufanya mazoezi na kuzingatia mtindo bora wa maisha, pamoja na huduma za Afya ya Uzazi na uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi.

“Katika bonanza hili tutawafikia vijana kupitia michezo na kuwapatia elimu mbalimbali za afya, ikiwemo afya ya uzazi, lishe na UKIMWI. Pia, tunalenga kuhamasisha vijana kuwa na mwitikio wa kuhudhuria vituo vya kutolea huduma za afya. Matarajio yetu ni kuwafikia zaidi ya vijana 3,000,” amesema Kihwele.

Ameeleza kuwa bonanza hilo ni fursa muhimu kwa ajili ya kuongeza uelewa wa vijana kuhusu afya ya uzazi, kuzuia magonjwa yanayohusiana na afya ya uzazi na kuchangia kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika kupitia elimu, kinga na upatikanaji wa huduma za afya kwa wakati.

Kwa upande wake, Mratibu wa Afya ya Uzazi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bi. Betha Yohana, amesema bonanza hilo litahusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, kukimbia na yai, kukimbia na magunia, kuvuta kamba, Kukimbiza Kuku na kuibua vipaji vya uimbaji, ikiwa ni njia ya kuwavutia vijana kushiriki na kupata elimu ya afya kwa mazingira rafiki. Aidha, amewahimiza vijana kutoka vyuoni, shuleni na wale waliopo uraiani kujitokeza kwa wingi kunufaika na fursa hiyo.

Ameongeza kuwa huduma za afya zitatolewa bure kwa siku zote tatu za bonanza hilo, zikiwemo uzazi wa mpango, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na upimaji wa uzito, pamoja na huduma nyingine zitakazozingatia mahitaji ya vijana.