Customer Feedback Centre

Ministry of Health

ACHENI MATUMIZI HOLELA YA DAWA - WAZIRI UMMY

Posted on: June 19th, 2024



Na WAF - Arusha


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kuacha matumizi holela holela ya Dawa ili kuepuka usugu wa vimelea dhidi ya dawa hususani za antibaotik kushindwa kufanya kazi ipasavyo na kugharimu maisha na nguvu kazi ya Taifa.


Waziri Ummy amesema hayo leo Juni 19, 2024 Jijini Arusha wakati wa kilele cha maadhimisho ya Miaka 50 ya Jumuiya ya Afya ya nchi zacMashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) ambapo mgeni Rasmi alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango.


"Usugu wa vimelea vya magonjwa Dhidi ya Dawa ni janga kubwa ambalo jamii ya Watanzania inapaswa kupambana nalo kwa dhati kwa kuwa madhara yake ni makubwa na yanagharimu fedha nyingi." Amesema Waziri Ummy


Amesema, ikiwa umeandikiwa dawa unywe kwa siku Tano basi maliza siku zote Tano, zingatia matumizi sahihi ya dawa hususani za antibaiotik na usitumie dawa bila ya kuandikiwa na daktari au mtaalam wa mifugo, unakuta dawa za mifugo anapewa binaadamu tuepuke kutengeneza janga kubwa ambalo litakwenda kugharimu Sekta ya Afya kwa siku za usoni kwa kuendelea na matumizi holela ya dawa." Amesema Waziri Ummy


"kuongezeka kwa mzigo wa magonjwa Yasiyoambukiza katika ukanda huu, Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) imejipanga kuja na Tafiti zitakazo saidia kuja na ushahidi wa kisayansi utakao saidia mbinu sahihi za kupambana na magonjwa hayo na kuweka sera nzuri zitakazosaidia kufikia suala la Afya kwa wote.


Aidha, Waziri Ummy amesema katika miaka 50 ya Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) kuna mengi makubwa ya kujivunia kwa kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikitoa msaada wa kiufundi katika masuala ya afya na nchi za ukanda wa mashariki, kati na kusini mwa Afrika wataendelea kuongeza mashrikiano baina ya nchi wanachama ili kubuni na kuendeleza afua zaidi za Afya ambazo zitasaidia kukabiliana na changamoto zinazoikabili Sekta hiyo barani Afrika.