Ministry of Health

WAZIRI MCHENGERWA AGHARAMIA VIFAA KWA WATOTO 15 WENYE CHANGAMOTO YA USIKIVU

Posted on: July 25th, 2026

Na Andrea Kadege, WAF-Arusha

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amegharamia vifaa kwa watoto 15 waliogundulika na changamoto ya usikivu katika kambi ya madakatari bingwa wa upasuaji inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru.

Hayo yamebainishwa leo Julai 25, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe alipokuwa akikagua utoaji wa huduma za afya na kuzungumza na Madaktari Bingwa na Bobezi wanaoshiriki kambi ya huduma za kibingwa ya upasuaji iliyoratibiwa na ECSA HC na wadau wengine inayoendelea hospitalini hapo.

"Mhe. Mchengerwa ameagiza kuandaliwa kwa taarifa kamili za watoto hao 15, ikiwemo majina, maeneo wanakotoka pamoja na gharama za vifaa wanavyohitaji, ili mchakato wa kuwapatia msaada huo ukamilike kwa wakati" amesema Dkt Magembe

Katika hatua nyingine, Dkt. Magembe amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya kinga kwa wananchi ili kupunguza idadi ya watu wanaopata matatizo ya usikivu yanayoweza kuzuilika.

Amesema wananchi wanaofanya kazi katika mazingira yenye kelele nyingi, ikiwemo viwandani, migodini na maeneo mengine ya uzalishaji, wanapaswa kuhamasishwa kutumia vifaa kinga binafsi vinavyolinda masikio dhidi ya kelele kali zinazoweza kuharibu uwezo wa kusikia.

Dkt. Magembe amepongeza wadau wa maendeleo na madaktari bingwa na bobezi wanaoshiriki kambi hiyo kwa huduma wanazoendelea kutoa, akisema zimeleta matumaini kwa wananchi wengi wanaohitaji huduma za kibingwa karibu na makazi yao.