Ministry of Health

KIBITI YAIMARISHA UTAYARI KUKABILI EBOLA NA EL NINO

Posted on: September 24th, 2026

Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Mkoani Pwani, imeimarisha utayari wa kukabiliana na tishio la Ebola na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na El Nino, huku wananchi wakipewa elimu ya namna ya kuchukua tahadhari mapema.

Akizungumza katika ziara ya uhamasishaji na ushirikishwaji wa jamii leo Septemba 24, 2026, Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt. Dismas Masulubu, amesema wananchi wamekuwa wakipewa taarifa kupitia vikao mbalimbali, ikiwemo kuelekezwa kuondoka maeneo yenye hatari ili kupunguza madhara wakati wa dharura.

“Moja ya mambo ambayo tumeyafanya ni kutoa taarifa kwa wananchi kupitia vikao vyetu, tumewaelekeza kuweza kuondoka maeneo yenye hatari zaidi ili kupunguza athari,” amesema Dkt. Masulubu.

Kwa upande wake, Afisa kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Francis Marwa, amesema uelewa wa jamii ni muhimu katika kutambua viashiria vya hatari, kutoa taarifa kwa wakati na kuchukua hatua stahiki.

Mafunzo hayo yamejikita katika utambuzi wa dalili, kinga na udhibiti wa maambukizi, matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga pamoja na hatua za kuchukua wakati wa dharura.

Zoezi hilo linatekelezwa na Wizara ya Afya kupitia Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu–Sera, Uratibu na Bunge pamoja na UNICEF, Save the Children na TIP, likilenga kuimarisha utayari wa Halmashauri na jamii kukabiliana na Ebola na athari za El Nino.