Ministry of Health

SHINYANGA MC YAWEKA MKAZO WA TAHADHARI YA AFYA MIGODINI, MACHIMBONI DHIDI YA EBOLA NA EL NINO ‎

Posted on: September 25th, 2026

Na WAF-SHINYANGA.
‎
Wilaya ya Shinyanga imeweka mkazo katika kuhakikisha tahadhari za afya na usalama dhidi ya mvua kubwa za El Niño pamoja na magonjwa ya kuambukiza, ikiwemo Ebola, zinafika pia katika maeneo ya migodi na machimbo ambako wananchi wanafanya shughuli za uchimbaji.
‎
‎Hatua hiyo imeelezwa wakati timu kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Rais–TAMISEMI ilipokutana na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Julius Mtatiro, kujadili maandalizi ya Wilaya katika kukabiliana na majanga na kulinda afya na usalama wa wananchi.
‎
‎Akizungumza katika kikao hicho leo Septemba,2025 Wilayani Shinyanga, Mhe. Julius Mtatiro Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga amesema Wilaya imeendelea kufanya ziara katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchunguzi na kutoa elimu kwa wananchi, wakiwemo wanaoishi mabondeni pamoja na wale wanaofanya shughuli za uchimbaji katika maeneo ya migodi.
‎
‎Amesema katika kipindi cha mvua kubwa za El Niño, wananchi wanaofanya shughuli za uchimbaji wanapaswa kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mamlaka ya hali ya hewa kutokana na hatari zinazoweza kujitokeza katika maeneo ya machimbo, ikiwemo maji kujaa katika maeneo ya uchimbaji, mmomonyoko wa ardhi na hali nyingine zinazoweza kuhatarisha maisha.
‎
‎Mhe. Mtatiro amesisitiza umuhimu wa wachimbaji na wananchi wanaoishi katika maeneo ya migodi kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuchukua hatua za tahadhari mapema pale kunapotolewa taarifa kuhusu mvua kubwa au hali nyingine hatarishi.
‎
‎ Aidha,kwa upande wa afya, ameeleza kuwa Wilaya inaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, huku akiwataka wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya na mamlaka husika endapo kutatolewa tahadhari kuhusu ugonjwa wa Ebola au magonjwa mengine.
‎
‎Mhe. Mtatiro amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kupata taarifa sahihi kutoka kwenye mamlaka husika, akieleza kuwa taarifa zinazotolewa kwa wakati zina mchango mkubwa katika kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa majanga na dharura.