TANZANIA, NEXLEAF KUENDELEZA TEKNOLOJIA YA USIMAMIZI WA CHANJO NCHINI
Posted on: September 25th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF – New York
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, ameishukuru Nexleaf Analytics kwa mchango wake wa kuimarisha usimamizi wa chanjo nchini akieleza kuwa matumizi ya teknolojia na data yamekuwa muhimu katika uhifadhi wa chanjo kwa viwango vinavyotakiwa na kulinda ubora katika mnyororo mzima wa ugavi.
Dkt. Magembe ameyasema hayo Septemba 24, 2026 jijini New York, Marekani katika mkutano wa pembeni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA), uliojadili ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Nexleaf Analytics katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa chanjo.
Amesema, kupitia ushirikiano huo ulioanza mwaka 2017 na kuimarishwa zaidi kupitia Mkataba wa Makubaliano (MoU) uliosainiwa mwaka 2019, Nexleaf imewezesha Tanzania kutumia vifaa vya ufuatiliaji wa halijoto ya chanjo kwa njia ya mbali (Remote Temperature Control Devices), hatua iliyosaidia kuongeza matumizi ya data katika kufanya maamuzi kuhusu utendaji na matengenezo ya vifaa.
Aidha, Dkt. Magembe amesema Tanzania imeendelea kutumia ubunifu huo katika kuimarisha usimamizi wa vifaa kupitia mfumo wa kielektroniki wa MEIMIS-CCE ambao unasaidia kutuma taarifa za halijoto kufanya maamuzi kuhusu matengenezo na kuongeza muda wa matumizi ya vifaa vya mnyororo baridi.
Katika kuendeleza ushirikiano huo, Dkt. Magembe ameiomba Nexleaf kuendelea kusaidia maboresho na matengenezo ya mifumo ya RTMD na MEIMIS-CCE, matumizi ya teknolojia na ubunifu katika usimamizi wa vifaa vya mnyororo baridi pamoja na upatikanaji wa vifurushi vya data kwa ajili ya RTMDs na mafunzo kwa wataalamu wa ndani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi na mwanzilishi wa Nexleaf Analytics Dkt. Nithya Ramanathan, amesema wako tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania na kwamba watafika nchini kuanzia Septemba 30, 2026, ambapo wataangalia hali halisi ya mifumo hiyo na kuweka mpango mkakati wa namna ya kutekeleza maombi ya Tanzania.