Ministry of Health

MJI WA MAFINGA WAWEKA MAAZIMIO KUIMARISHA UTAYARI WA KUKABILIANA NA EL NIÑO, EBOLA

Posted on: September 26th, 2026

Na Atley Kuni, WAF – Mafinga, Iringa

Halmashauri ya Mji wa Mafinga imeweka maazimio tisa yenye lengo la kuimarisha utayari na uwezo wa kukabiliana na athari za mvua ya El Niño pamoja na magonjwa ya milipuko, ikiwemo Ebola.

Akizungumza Septemba 26,2026 wakati wa zoezi la kuimarisha utayari wa kukabiliana na Ebola na Uelekeo wa Mvua za El niño, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Dkt. Bonaventura Chitopela, amesema maazimio hayo yamelenga kuhakikisha watumishi na vituo vya kutolea huduma za afya wanakuwa tayari kutambua, kutoa taarifa na kuchukua hatua kwa wakati endapo kutatokea dharura ya afya kwa umma.

Dkt. Chitopela ameahidi kuyachukua maazimio hayo na kuyafanyia kazi ili kuendelea kuimarisha mfumo wa utayari wa Halmashauri kukabiliana na dharura

Kwa upande wake, Mratibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Chipole Mpelemba, amesisitiza umuhimu wa kuwa na utayari wakati wote, akieleza kuwa maandalizi hayo yanapaswa kuzingatia miongozo na mtiririko wa hatua zinazotakiwa kuchukuliwa kabla, wakati wa dharura na hata baada ya dharura.

Amesema, kuwa na utayari mapema ni muhimu katika kuhakikisha athari za majanga na magonjwa ya milipuko zinadhibitiwa kwa ufanisi.

Hatua hizo ni sehemu ya jitihada zinazoendelea kutekelezwa za Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na Wadau mbalimbali za kuimarisha utayari wa vituo vya afya kukabiliana na dharura za afya ya umma, ikiwemo Ugonjwa wa Ebola na uelekeo wa mvua za El niño zinazo tabiriwa kuanza kunyesha hivi karibuni.