Ministry of Health

DKT. SAMIZI: MAABARA NDIYO UTI WA MGONGO WA MATIBABU

Posted on: September 24th, 2026

Na Arcad Mosha, WAF – Mbeya

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence George Samizi, amesema huduma za maabara ni msingi muhimu katika utoaji wa huduma bora za afya, akiwataka wataalamu wa maabara kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na kwa wakati ili kuendelea kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.

Dkt. Samizi ameyasema hayo leo Septemba 24, 2026 jijini Mbeya wakati akimwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, katika ufunguzi rasmi wa Kongamano la 39 la Kisayansi la Chama cha Wataalamu wa Maabara (MeLSAT), lililofanyika katika Ukumbi wa City Park Garden.

Amesema Serikali, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuchukua hatua za kuimarisha huduma za maabara nchini, ikiwemo kushughulikia changamoto ya upungufu wa wataalamu kupitia mchakato wa mapitio ya ikama za kada za afya.

“Maabara ndiyo uti wa mgongo wa matibabu, Ni muhimu wataalamu wa maabara kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi, uaminifu na kwa wakati ili huduma zinazotolewa ziwe na ubora na wananchi waweze kunufaika,” amesema Dkt. Samizi.

Akizungumzia changamoto ya muundo wa uongozi katika huduma za maabara, amesema Wizara ya Afya inaendelea kufanya maboresho ya mifumo na miongozo ya usimamizi wa huduma hizo ili kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha majukumu ya kitaalamu na kiutawala yanaeleweka na kutekelezwa ipasavyo.

Dkt. Samizi amesema Serikali kupitia Baraza la Wataalamu wa Maabara inaendelea na mchakato wa mapitio ya Sheria Na. 22 ya Mwaka 2007, ambapo imependekezwa wataalamu wenye Shahada ya Maabara kufanya mafunzo ya utarajali kwa miezi 12 katika vituo vinavyotambuliwa kabla ya kusajiliwa.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuweka mifumo ya kuhakikisha vipimo vya haraka vinavyofanywa na watoa huduma waliopewa mafunzo vinafanyika kwa kuzingatia viwango vya ubora, huku ikiendelea kuajiri na kuongeza wataalamu wa maabara katika kada na ngazi mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya huduma nchini.