Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATAALAMU WA AFYA WEKEZENI UJUZI WENU KUWASAIDIA WANANCHI

Posted on: May 7th, 2024



Na WAF - Njombe

Wataalamu wa Afya nchini wametakiwa kuwekeza nguvu zao kuwahudumia wananchi, kwakuwa serikali imeweka mazingira rafiki na wezeshi ya kutoa huduma bora.

Wito huo umetolewa Mei 6, 2024 na Mkuu wa wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda katika hafla ya kuwapokea Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia Suluhu Hassan wapatao 30, katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Njombe, akimwakilisha Mhe. Anthony Mtaka

"Katika mkoa wetu, Mheshimiwa Rais ametoa fedha nyingi za kujenga vituo vya afya, vipo takribani vituo sita vipya, hivyo tunaomba serikali kupitia Wizara ya Afya izidi kuwekeza katika kuwaleta madaktari kwenye maeneo yetu ikiwemo madaktari bingwa katika maeneo yetu"

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dkt. David Ntaindwa ameshauri wataalamu hao hasa wanaotoa huduma za Kibingwa za watoto kutoa elimu kwa wazazi, kuhusu lishe bora ili kuendelea kupunguza hali ya Udumavu mkoani humo.

Mratibu wa mpango kabambe wa Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia, Jackline Ndanshau amesema kuwa wizara ya Afya imejipanga kuhakikisha fedha alizotoa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinatumika kuwahudumia wananchi kama ilivyokusudiwa.

Miongoni mwa madaktari waliofika Njombe ni Dkt. Elenestina Mwipopo, Daktari Bingwa Mbobezi wa watoto wachanga amewataka wakazi wa Njombe kutoa ushirikiano kwa kipindi ambacho watakuwepo mkoani Njombe kutoa huduma.

"Njombe ni mkoa wenye vyakula vingi, hivyo tumekuja kutibu lakini kutoa elimu ya namna wananchi wa mkoa wa Njombe wanavyopaswa kutumia uwepo wa vyakula hivi ili kuondokana na tatizo la Udumavu kwa kuwa makundi yote muhimu ya vyakula yanazalishwa mkoani hapa. Amesema Dkt. Mwipopo.

Kampeni Kabambe ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Njombe itadumu kwa siku tano ikiwa imeanza leo Mei 6 hadi Mei 10 mwaka huu katika Hospitali zote sita za Halmashauri za Wilaya ndani ya Mkoa wa Njombe.