Ministry of Health

TANZANIA, CANADA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA,WADAU BINAFSI KUTUMIKA

Posted on: March 14th, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Vifaa Tiba na Dawa, Bw. Emmanuel Tayari, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Canada unalenga kuimarisha Huduma za afya kwa wananchi kupitia ushirikishwaji wa sekta binafsi.

Bw. Tayari amesema hayo leo, Machi 12, 2026, katika kikao kilichokutanisha Serikali za Tanzania na Canada, sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo jijini Dar es Salaam.

“Ushirikiano huu unalenga kukuza utambuzi wa utaalamu wa Canada katika teknolojia za afya pamoja na ubunifu wa vifaa tiba.

"Hatua hii itasaidia kuimarisha huduma za afya, kuongeza ubora wa matibabu, na kuchochea ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya sekta ya afya nchini,” amesema Bw. Tayari.

Ameongeza kuwa Tanzania imeimarisha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya afya kwa kuweka sera na mifumo rafiki inayowezesha ushiriki wa sekta binafsi.

Aidha, Bw. Tayari amesema kuwa kuongeza uelewa kuhusu taratibu za udhibiti na mazingira ya biashara katika sekta ya afya ni muhimu ili kuhakikisha wawekezaji wanapata mwongozo sahihi juu ya jinsi ya kuendesha shughuli zao kimaadili na kwa mujibu wa sheria. Hatua hii pia inahakikisha ubora wa bidhaa na huduma za afya.

Kwa upande wake, Balozi wa Canada nchini Tanzania amesema serikali ya Canada inaendelea kushirikiana na Tanzania katika juhudi za kuboresha huduma za afya, ikiwemo kuimarisha uwezo wa kitaalamu, kutoa msaada wa kifedha na kiufundi, pamoja na kukuza teknolojia za kisasa na ubunifu wa vifaa tiba.

"Ushirikiano huu unaonyesha dhamira thabiti ya pande zote mbili katika kuhakikisha sekta ya afya nchini Tanzania inakua kwa njia endelevu, ikileta manufaa kwa wananchi wote, huku ikichangia katika kujenga mazingira ya kibiashara yanayowezesha uvumbuzi na kuongeza ajira.

Shabaha ya kikaonhicho ilikuwa kubadilishana uzoefu kuhusu vipaumbele vya sekta ya afya nchini Tanzania, mazingira ya udhibiti na biashara, pamoja na kutambua fursa za ushirikiano, hususan katika suluhisho zinazotolewa na sekta binafsi.