UONGOZI UNAOBADILIKA WAWEZESHA MAGEUZI YA HUDUMA ZA AFYA
Posted on: March 17th, 2026Na Said Nyaoza, WAF – Arusha
Serikali imesisitiza umuhimu wa kutumia mbinu za uongozi unaoendana na mabadiliko ya mazingira ili kuimarisha mfumo wa utoaji huduma za afya na kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Akifungua mafunzo ya uongozi kuhusu utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI Machi 16, 2026 jijini Arusha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Bw. Ismail Rumatila, amesema mbinu hiyo ya uongozi itawasaidia viongozi na wadau wa afya kusimamia mabadiliko yanayohitajika ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Amesema uongozi unaoendana na mabadiliko ya mazingira (Adaptive Leadership) huwasaidia viongozi kutofautisha changamoto za kiufundi zinazoweza kutatuliwa kwa utaalamu au taratibu zilizopo na changamoto za kimfumo zinazohitaji mabadiliko ya fikra, tabia na ushirikiano mpana.
“Changamoto nyingi tunazokutana nazo katika sekta ya afya hazihitaji suluhisho la kiufundi pekee, bali zinahitaji uongozi unaoweza kuhamasisha watu kujifunza kutokana na uzoefu na kusaidia taasisi kuendana na mabadiliko ya mfumo wa afya,” amesema Bw. Rumatila.
Ameongeza kuwa Serikali imeweka mkakati madhubuti wa kuimarisha mfumo wa afya kupitia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, kuboresha huduma za afya ya msingi pamoja na kuongeza uwajibikaji na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu Bw. Rumatila, mafanikio ya mpango wa huduma ya afya kwa wote yatapimwa kwa kiwango ambacho wananchi watapata huduma bora kwa urahisi na familia kulindwa dhidi ya gharama kubwa za matibabu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Miradi wa Global Fund Makao Makuu Geneva, Bi. Sarah Asiimwe, amesema maandalizi ya mafunzo hayo yalianza tangu mwaka 2018 lakini utekelezaji wake umefanikiwa sasa kutokana na dhamira ya Serikali ya Tanzania kuimarisha programu za afya zinazoungwa mkono na taasisi hiyo.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo ni muhimu kwenye kuhakikisha mipango ya afya inatekelezwa kwa ufanisi na kufanikisha lengo la huduma bora za afya kwa wote.
Bi. Asiimwe pia amepongeza Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Wizara ya Afya kwa ushirikiano wao wa kuimarisha usimamizi