Ministry of Health

WIZARA YA AFYA, WADAU WAKUTANA KUANDAA MPANGO ENDELEVU SEKTA YA AFYA

Posted on: March 15th, 2026

Na Emmanuel Malegi, WAF- Morogoro

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo CHAI na FCDO inaandaa Mpango wa Uendelevu wa Sekta ya Afya kupitia taarifa ya tathmini ya uendelevu wa utoaji wa huduma za afya nchini pamoja na kuweka mikakati ya kuhakikisha huduma bora za afya zinakuwa endelevu.

Akielezea malengo ya kikao hicho Machi 12, 2025 Mkoani Morogoro, Dkt. Hussein Athumani ambaye ni mratibu wa dawati la uimarishaji wa mifumo ya afya amesema Wizara ya Afya kupitia Idara ya Sera na Mipango inaendelea na utekelezaji wa mchakato wa kuandaa Mpango wa Taifa wa Uendelevu wa Sekta ya Afya (NHSSP), hivyo ni vyema kukutana na wadau kuandaa mpango huu muhimu kwa pamoja.

“Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo katika kuboresha huduma za afya nchini, huduma hizi zinapaswa kuwa endelevu na stahimilivu ili kuwezesha upatikanaji wake wakati wote’’, amesema Dkt. Hussein.

Ameongeza kuwa kwa muktadha huo, ndiyo maana wamekutana hapo ili washirikiane kwa pamoja katika kupitia matokeo ya tathmini iliyofanyika na kuja na mikakati ya kuhakikisha uendelevu wa utoaji wa huduma bora za afya kwa jamii

Naye Mkrugenzi Mkaazi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Clinton Health Access Initiatives (CHAI) Dkt. Esther Mtumbuka amesema kikao hcho ni hatua muhimu ya kuisaidia Serikali kuwa na mkakati mahiri kuhakikisha uendelevu wa huduma zilizokua zinafadhiliwa na Wadau zinaendelea.

Dkt. Esther ameongeza kuwa katika kipindi dunia inapitia kipindi cha mabadiliko ya kiuchumi, Taasisi ya CHAI inaendelea kusaidiana na Serikali katika kutekeleza mpango huo unaoandaliwa kwa kuchambua maeneo ya kipaumbele yanayotakiwa kutiliwa mkazo ikiwa pamoja na kuainisha vyanzo vipya vya mapato.