Ministry of Health

UJENZI WA JENGO LA WAGONJWA WA NJE MOI KUPUNGUZA MSONGAMANO WA WAGONJWA

Posted on: March 15th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Dar es Salaam

Serikali imesema ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) utasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa pamoja na kuongeza ubora na ufanisi wa huduma za tiba nchini.

Hayo yameelezwa Machi 14, 2026 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI katika taasisi hiyo, ambapo alipo mwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Samizi amesema mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 13 na ulianza kutekelezwa Septemba 2, 2024 huku ukitarajiwa kukamilika Agosti 19, 2026 likiwa ni jengo lenye sakafu tano likiwa na vyumba 45 vya madaktari kwa ajili ya huduma za uchunguzi, vyumba 10 vya upasuaji, huduma za mazoezi tiba pamoja na eneo la maegesho ya magari katika sakafu ya chini.

Aidha, Amesema lengo la mradi huo ni kupunguza msongamano uliopo kwa wagonjwa wa nje, kuongeza uwezo wa kuhudumia wagonjwa wengi zaidi, kuboresha ubora wa huduma za tiba pamoja na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya taasisi ambapo kwa sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 54, na ukikamilika jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa kati ya 700 hadi 800 kwa siku bila kusababisha msongamano.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lukumay amewataka watumishi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili kuendelea kutoa huduma kwa weledi huku wakitumia lugha zenye staha na heshima kwa wagonjwa ili kuimarisha mahusiano mema kati ya wahudumu wa afya na wananchi wanaofika kupata huduma.