Ministry of Health

WATAALAMU WA AFYA WAFANYA TATHMINI YA UTAYARI WA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MILIPUKO KAGERA

Posted on: August 18th, 2026

Na Happyness Hans, WAF - Kagera

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Rebecca Gwambasa, amesema ugeni kutoka Wizara ya Afya na wadau kutoka Shirika la usalama wa afya Duniani CIHEB umefika mkoani Kagera kwa ajili ya kuangalia namna mkoa ulivyojiandaa kukabiliana na magonjwa ya milipuko pamoja na kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya katika vituo mbalimbali na kufanya tathmini ya Viwango vya Kitaifa na Kimataifa vya Kukinga na Kudhibiti Maambukizo (IPC) katika hospitali za mkoa.

Amesema hayo leo Agosti 18, 2026 mkoani Kagera wakati akiwapokea wataalamu hao watakaofanya ufuatiliaji wa masuala ya IPC pamoja na huduma za matibabu kwa watu walioambukizwa magonjwa, huku wakiwajengea uwezo watumishi wa afya ili wawe tayari kukabiliana na magonjwa ya milipuko.

Dkt. Gwambasa amesema mkoa umelipokea vizuri zoezi hilo kwa kuwa Kagera imezungukwa na nchi jirani ambazo baadhi tayari zimekumbwa na magonjwa ya milipuko, hivyo hatua hiyo itasaidia wananchi kupata huduma bora za afya pindi magonjwa hayo yanapotokea.

Kwa upande wake, Mratibu wa IPC kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Chrisogone German, amesema lengo la zoezi hilo ni kufanya tathmini katika eneo la kukinga na kudhibiti maambukizi (IPC) katika hospitali zote za Halmashauri za Mkoa wa Kagera, tathmini hiyo itasaidia kubaini maeneo yanayohitaji maboresho katika kinga na udhibiti wa maambukizi.

Aidha, amesema wataalamu hao watawajengea uwezo watoa huduma za afya ili waweze kukabiliana ipasavyo na wagonjwa wa magonjwa ya milipuko endapo yatatokea. Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha vituo vya afya vinakuwa tayari kutoa huduma kwa usalama na ufanisi wakati wa milipuko.

Naye Muuguzi kutoka Kituo cha Afya Rusumo ameishukuru timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya kwa kufika katika kituo hicho na kuangalia namna walivyojiandaa kukabiliana na magonjwa ya milipuko. Amesema uwepo wa wataalamu hao umewapa fursa ya kupata elimu na ushauri kuhusu namna bora ya kukabiliana na milipuko.