Ministry of Health

WATAALAM WA AFYA WAFANYA TATHMINI YA UTAYARI WA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MILIPUKO BIHARAMULO

Posted on: August 20th, 2026

Na Happyness Hans, WAF – Kagera

Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha Uhakiki ubora wa huduma za afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, pamoja na wadau kutoka CIHEB kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani, imefika mkoani Kagera kwa ajili ya kutathmini utayari wa mkoa katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko, kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya katika vituo mbalimbali, pamoja na kufanya tathmini ya viwango vya kitaifa na kimataifa vya Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi (IPC) katika hospitali za mkoa wa Kagera.

Hayo yamesemwa leo Agosti 20, 2026 na Mratibu wa tathmini ya viwango vya kitaifa na kimataifa vya kuzuia na kudhibiti maambukizi (IPC) katika Hospitali za Wilaya za Biharamulo na Ngara, Dkt. Bushi Lugoba, amesema timu ya wataalamu wa afya imefika Hospitalini hapo kufanya tathmini ya utekelezaji wa IPC, kubaini kiwango cha utekelezaji wa masuala hayo, pamoja na kuwawezesha watumishi ili kuboresha utekelezaji wa shughuli za IPC.

Dkt. Lugoba amesema zoezi hilo limefanyika vizuri kutokana na ushirikiano wa kutosha walioupata kutoka kwa watumishi wa hospitali hiyo, huku timu hiyo ikikamilisha tathmini na kutoa mrejesho kuhusu maeneo yaliyobainika kuwa na changamoto, pamoja na kuelekeza namna sahihi ya kufanya kazi katika maeneo hayo.

Amesema baada ya kukamilisha zoezi katika Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo, timu hiyo itaelekea Wilaya ya Ngara kuendelea na tathmini na kuwawezesha watumishi katika utekelezaji wa masuala ya kuzuia na kudhibiti maambukizi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo, Tumpale Akimu amesema amepokea vizuri zoezi hilo la timu kutoka Wizara ya Afya, akieleza kuwa mafunzo yanayotolewa kwa watumishi yanawasaidia kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kujikinga wao pamoja na wagonjwa, hasa katika kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza. Amesema baada ya mafunzo hayo, hospitali itaboresha maeneo yote yaliyobainika kuwa na changamoto.