Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WANAHABARI NI NGUZO MUHIMU YA UTOAJI ELIMU KWA JAMII KUHUSU UGONJWA WA POLIO.

Posted on: September 15th, 2023

Na WAF - Dodoma


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amewawaasa Waandishi wa Habari kuwa mabalozi katika utoaji wa elimu ya umuhimu wa Chanjo ya Matone dhidi ya Ugonjwa wa Polio kwani ni nguzo muhimu katika kuifikia jamii kwa haraka.


Senyamule amebainisha hayo leo Septemba 15 wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya Kitaifa na Mkoa wa Dodoma yenye lengo la kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kuandika Habari zenye tija katika uelemishaji juu ya ugonjwa wa Polio.


“Ninyi Wanahabari ni nguzo muhimu na mnaifikia jamii kwa uharaka hivyo nawaasa mkawe mabalozi katika kuelimisha jamii,nyie mkiamua mambo yafanikiwe inawezekana,mkiamua mambo yasifanikiwe inawezekana nichukue nafasi kuwapongeza ”amesema.


Aidha Senyamule amewaomba viongozi wa mikoa husika zoezi hilo la kampeni ya chanjo litakapofanyika kufuatilia kwa makini ili kufanya kwa ufanisi huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kuwapeleka watoto kupatiwa chanjo.


Akitoa mafunzo kwa wanahabari Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo Florian Tinuga amesema lengo la mafunzo hayo kwa wanahabari ni kuwezesha kupata elimu kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Polio na kuwezesha kupata uelewa juu ya kinga zake.


Aidha, ameainisha miongoni mwa dalili za ugonjwa wa Polio ni pamoja na kulemaa kwa ghafla, kulegea kwa kiungo, kukosa nguvu, kushindwa kunyanyua mguu au mkono ,mtoto kushindwa kukaa ambapo amesisitiza mtu yeyote aonapo dalili kama hizo wakati wa kampeni ya nyumba kwa nyumba ni muhimu kuhakikisha mtoto anapelekwa kwenye kituo cha kutolea huduma za afya kilichokaribu.


Halikadhalika ametoa ujumbe mahsusi kwa jamii kuendelea kuimarisha usafi, kunawa mikono mara kwa mara pamoja na kuendelea kuchukua tahadhari ili kujilinda na ugonjwa hatari wa Polio kwani unasababisha kupooza au ulemavu wa kudumu na hatimaye kifo kwani ni salama na haina madhara.


Ikumbukwe kuwa kampeni ya chanjo ya Matone dhidi ya Ugonjwa wa Polio inatarajiwa kuanza Septemba 21-24,2023 katika Halmashauri 37 kutoka mikoa 6 ya Kigoma, Kagera, Mbeya, Songwe, Katavi na Rukwa na walengwa ni watoto walio na umri chini ya miaka 8 na wanaotarajiwa kufikiwa ni 3,250,598.


Polio ni ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Polio, ugonjwa huu husababisha kupooza na baadaye kifo na Virusi vya Polio huingia mwilini kwa njia ya mdomo, kunywa maji, au chakula ambacho kimechafuliwa na kinyesi kutoka kwa mtu aliyeambukizwa kirusi hicho.