Ministry of Health

UJENZI WA UCHUMI IMARA WA AFYA AFRIKA MASHARIKI KUWA AJENDA KUU YA KONGAMANO LA EAHF 2026

Posted on: July 27th, 2026

Na Shaban Juma, Dar es Salaam

Ajenda ya kujenga uchumi imara wa afya Afrika Mashariki kupitia ushirikiano, uwekezaji na mifumo thabiti ya utoaji huduma za afya imepewa kipaumbele katika maandalizi ya Kongamano la 13 la Shirikisho la Watoa Huduma za Afya Afrika Mashariki (EAHF) na Maonesho ya Kimataifa ya Afya 2026, yatakayofanyika Agosti 21 hadi 23, 2026 jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Hayo yamejadiliwa leo Julai 27, 2026 kwenye kikao kati ya Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa na ujumbe kutoka nchini Ethiopia ulioongozwa na Rais wa Ethiopian Healthcare Federation (EHF) na Mkuu wa East African Healthcare Federation (EAHF), Dkt. Markos Feleke Haile, uliofika nchini kuwasilisha mwaliko rasmi wa ushiriki wa Tanzania katika kongamano hilo.

Akiongea katika kikao hicho, Dkt. Samizi amesema Tanzania inaendelea kuunga mkono juhudi za ushirikiano wa kikanda ili kuimarisha mifumo ya afya, kukuza uwekezaji, kuendeleza viwanda vya dawa na vifaa tiba pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

Ameongeza kuwa, ushiriki wa Tanzania katika kongamano hilo utatoa fursa ya kubadilishana uzoefu, kuonesha mafanikio ya sekta ya afya, kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali na kuvutia uwekezaji utakaochochea ukuaji wa uchumi wa afya kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

Dkt. Samizi amesema kaulimbiu ya kongamano hilo, "Resilience: Building the East African Health Economy," imekuja wakati muafaka huku nchi za Afrika Mashariki zikiendelea kuimarisha mifumo ya afya baada ya uzoefu uliotokana na changamoto za dharura za afya duniani.

Amesema kongamano hilo litatoa jukwaa muhimu kwa serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, taasisi za elimu, wawekezaji na wabunifu kujadiliana kuhusu suluhisho la kuboresha utoaji wa huduma za afya na kuharakisha ushirikiano wa kikanda.