Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TUZINGATIE USAFI KUDHIBITI TRAKOMA – DKT. NGAIZA

Posted on: January 19th, 2026

Wito umetolewa kwa jamii kuzingatia kanuni za usafi binafsi, ikiwemo kunawa mikono na uso kwa kutumia maji safi na tiririka, ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza yakiwemo Trakoma.

Wito huo umetolewa leo tarehe 19 Januari, 2026 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Benedicto Ngaiza, wakati akifungua mafunzo kwa Madaktari Bingwa wa Macho kuelekea Kambi Maalum ya Usawazishaji wa Vikope (Trakoma), Mkoani Mtwara.

“Ugonjwa wa Trakoma unatokana na uchafu na kutozingatia usafi binafsi. Mtu asiponawa uso wake mara kwa mara hujiweka katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu. Hivyo, katika kujikinga na Trakoma, ni muhimu kuzingatia usafi binafsi na usafi wa mazingira,” amesisitiza Dkt. Ngaiza.

Aidha, Dkt. Ngaiza ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa ya kambi hiyo maalum, itakayo anza tarehe 20 na kuhitimishwa tarehe 24 Januari, 2026 katika Wilaya ya Tandahimba.

“Nitoe wito kwa wananchi kujitokeza kupata huduma hii muhimu ya usawazishaji wa vikope, ambayo inatolewa bila malipo. Nawashukuru wadau wote waliowezesha kufanyika kwa zoezi hili lenye manufaa makubwa kwa afya ya macho,” amesema.

Ikumbukwe kuwa Kambi Maalum ya Usawazishaji wa Vikope (Trakoma) katika Wilaya ya Tandahimba, Mkoa wa Mtwara, itafanyika katika vituo mbalimbali vya afya ikiwemo Kituo cha Afya Michinji (tarehe 18), Kituo cha Afya Mkola Chini (tarehe 21), Kituo cha Afya Kigamboni (tarehe 22) na Kituo cha Afya Luagala (tarehe 23 Januari, 2026).

Huduma hizo zitatolewa bila malipo, na wananchi wote wanakaribishwa.