Customer Feedback Centre

Ministry of Health

LISHE BORA, MAZOEZI MTINDO BORA WA KUJIKINGA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

Posted on: January 10th, 2026

Na WAF – Arusha

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amewahimiza wananchi kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya ikiwemo kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kula vyakula vyenye lishe bora, kupunguza matumizi ya pombe na bidhaa za tumbaku pamoja na kujenga tabia ya kufanya mazoezi ili kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Dkt. Samizi ametoa wito huo leo Januari 09, 2026 jijini Arusha wakati akifunga rasmi kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo iliyofanyika katika hospitali ya Arusha, Lutheran Medical Center (ALMC) – Selian, kwa ushirikiano na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

"Kwa niaba ya Waziri wa Afya tunamshukuru kwa dhati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusogeza huduma za ubingwa na ubobezi za magonjwa ya moyo karibu na wananchi wa Mkoa wa Arusha na Kanda ya Kaskazini kwa ujumla," amesema Dkt. Samizi

Aidha, Dkt. Samizi ameeleza kuwa kusogezwa kwa huduma hizo mkoani Arusha ni hatua muhimu ikizingatiwa mkoa huo ni kitovu cha utalii na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Dkt. Samizi amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa vifo milioni 17.5 sawa na asilimia 32 ya vifo vyote Duniani husababishwa na magonjwa ya moyo, ambapo nchini Tanzania ikiwemo Mkoa wa Arusha una idadi kubwa ya wananchi wanaokabiliwa na ugonjwa huo.

Ameongeza kuwa magonjwa yasiyoambukiza kama magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, kisukari na saratani yanaendelea kuleta mzigo mkubwa wa kiafya na kiuchumi kwa jamii, hali inayohitaji jitihada za pamoja za Serikali, wadau wa afya na wananchi wenyewe katika kuyazuia na kuyadhibiti magonjwa hayo.