Ministry of Health

KATIBU TAWALA DODOMA AZITAKA RHMT, CHMT KUSIMAMIA IPASAVYO MRADI MPYA WA SBBC

Posted on: March 6th, 2026

Na Mvuda Jaffer ,WAF-Dodoma

Katibu Tawala wa mkoa wa Dodoma Dkt. Khamis Kazungu amewataka watendaji wa sekta ya afya mkoani hapo kuhakikisha Mradi wa SBBC Plus unatekelezwa kwa ufanisi ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto wachanga.

Akiongea Machi 05, 2026 wakati katika kikao cha utambulisho wa mradi huo, amesisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti na uwajibikaji katika ngazi zote za utekelezaji.

Dkt. Kazungu amesema kuwa, mradi huo wa miaka mitatu unaotekelezwa na Wizara ya Afya katika mikoa mitano ya Dar es Salaam, Morogoro, Simiyu, Kigoma na Dodoma, unalenga kuboresha huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto mchanga kwa kuimarisha ubora wa huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Kwa mujibu wa hotuba yake, utekelezaji wa mradi unahusisha usambazaji wa vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya pamoja na utoaji wa mafunzo na mafunzo elekezi kazini kwa watoa huduma ili kuhakikisha huduma zinazingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.

"Licha ya kupungua kwa takwimu za vifo vya uzazi kutoka vifo 74 mwaka 2024 hadi 57 mwaka 2025, na vifo vya watoto wachanga kutoka 433 hadi 290 katika kipindi hicho, bado juhudi zaidi zinahitajika ili kuondoa kabisa vifo vinavyozuilika" amesema Dkt. Kazungu.

Kwa upande wa mkoa wa Dodoma jumla ya vituo vya mfano 28 vimechaguliwa kushiriki kwenye mradi huo, vikitarajiwa kuwa kitovu cha utekelezaji bora wa huduma za wajawazito, huduma wakati wa kujifungua, huduma za watoto wachanga na huduma baada ya kujifungua.

Katibu Tawala ameziagiza timu za Usimamizi wa Afya za ngazi ya mkoa na halmashauri kuhakikisha mradi unaingizwa kikamilifu katika mipango ya afya, kufuatilia utekelezaji wake na kuwasilisha taarifa za maendeleo mara kwa mara.

Aidha, wasimamizi wa vituo vya afya wametakiwa kuhakikisha vifaa vinatumika na kutunzwa ipasavyo ili kuleta matokeo chanya yaliyokusudiwa.

Akihitimisha hotuba yake amesema kuwa Sekretarieti ya mkoa itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya na wadau wengine ili kuhakikisha ndani ya miaka mitatu ya utekelezaji, mabadiliko chanya yanaonekana katika viashiria vya afya ya uzazi na mtoto kwa mkoa w