Ministry of Health

MABORESHO YA MITAALA YA VYUO VYA AFYA KUIMARISHA UFUATILIAJI WA MAGONJWA NCHINI.

Posted on: March 10th, 2026

Serikali imeanza hatua za kuboresha mitaala ya vyuo vya afya ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi sahihi wa kutambua, kufuatilia na kutoa taarifa za magonjwa yaliyopewa kipaumbele, hatua inayotarajiwa kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa nchini.

Hatua hiyo inatekelezwa kupitia Mafunzo ya (Standardised Addendum) katika moduli za ufuatiliaji wa magonjwa, ambayo itatumika katika mitaala ya vyuo vya afya kwa kada za kati pamoja na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.

Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo yaliyofanyika mkoani Morogoro, Afisa Programu kutoka Wizara ya Afya , Idara ya Kinga, Kitengo cha Epidemiolojia na Udhibiti wa Magonjwa, Dkt. Frank Jacob amesema kuwa lengo la maboresho hayo ni kuhakikisha wanafunzi wanaosoma vyuo vya afya wanapata maarifa yanayolingana na mahitaji halisi ya mfumo wa afya nchini.

Amesema kuwepo kwa maudhui yanayofanana katika vyuo mbalimbali kutasaidia kuandaa wahudumu wa afya wenye uelewa wa pamoja kuhusu ufuatiliaji wa magonjwa yaliyopewa kipaumbele.

“Walimu wa vyuo wanapopata mafunzo haya wataweza kufundisha wanafunzi kwa ufanisi zaidi, hali itakayosaidia kuzalisha wahitimu wengi wenye uwezo wa kutumia mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa mara tu wanapoingia kazini,” amesema Dkt. Jacob.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani(WHO), Dkt. George Kauki, amesema kuwa maboresho ya mtaala yatasaidia kuongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu magonjwa ya mlipuko na namna ya kuyadhibiti.

Ameeleza kuwa kuwa na mitaala yenye maudhui yaliyoboreshwa kutawasaidia wanafunzi kupata ujuzi wa vitendo unaohitajika katika mfumo wa afya, hususan katika utambuzi na ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko.

Kikao hicho kimeratibiwa na Wizara ya Afya Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na Shirika la Afya Duniani(WHO) kikilenga kuhuisha na kuboresha maudhui ya mitaala ya mafunzo ya afya ili kuendana na mahitaji ya sasa ya ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa.