Customer Feedback Centre

Ministry of Health

JAMII YAHIMIZWA KUPEWA ELIMU YA MAGONJWA YA KUAMBUKIZA

Posted on: January 11th, 2026

Na, WAF- Dodoma

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amehimiza jamii kupewa elimu ya magonjwa ya kuambukiza kwa kuwafikia wananchi wa rika zote, hususan vijana, kwa kutumia mitandao ya kijamii kama njia kuu ya kufikisha ujumbe wa afya kwa haraka na kwa ufanisi.

Akizungumza leo tarehe 10 Januari, 2026,katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma, Dkt. Samizi ameyasema hayo wakati akipokea mawasilisho mbalimbali kutoka Vitengo, Idara na Programu za Wizara ya Afya, ikiwa ni mwendelezo wa kupata uelewa wa kina na taswira ya jumla kuhusu majukumu yanayotekelezwa ndani ya wizara

"Utoaji wa elimu ya afya unapaswa kuzingatia mbinu na njia ambazo makundi husika huzielewa na kuzisikiliza kwa urahisi, ili kuongeza uelewa na kuchochea mabadiliko chanya ya tabia katika jamii", amesema Dkt. Samizi

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwataka watendaji katika kila kitengo, idara na programu kutathmini na kubaini majukumu yanayowahusu ndani ya kipindi hicho na kuhakikisha yanatekelezwa ipasavyo.

Vilevile, Dkt. Samizi amewataka watendaji kwenda kutekeleza kikamilifu maelekezo yote Mhe. Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, yaliyotolewa ndani ya kipindi hicho kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Amesema azma ya Rais ni kuhakikisha mwananchi anasikilizwa na kusaidiwa, hivyo amezitaka idara, vitengo na programu kuhakikisha zina mifumo madhubuti ya kusikiliza na kupokea mrejesho wa wananchi pamoja na kuwa na uwezo wa kuwasaidia kutatua changamoto zao ili kuboresha utoaji wa huduma za afya.

Aidha, Dkt. Samizi ameelekeza kutumika kwa njia bora ya kutatua changamoto katika utoaji wa huduma za afya kwa kuwa na mifumo madhubuti ya kupokea malalamiko ya wananchi, kuyafanyia kazi kwa wakati na kutoa mrejesho unaoeleweka, hatua itakayoongeza imani ya wananchi katika huduma za afya.