Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TUNATAKA TUWE HURU KUZALISHA DAWA ZETU WENYEWE- WAZIRI MCHENGERWA

Posted on: January 19th, 2026

Na WAF, Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema kuwa uhamasishaji wa wawekezaji wa viwanda vya dawa nchini ni mpango wa Taifa ulioanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan shabaha ikiwa ni kuona Tanzania inajitosheleza kwa bidhaa hiyo lakini pia kuwa muuzaji kwa nchi zingine ifikapo 2030.

Waziri Mchengerwa amesema hayo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kando ya Kongamano la Wazalishaji wa Dawa pamoja na Vifaa tiba leo, Januari 19, 2026, katika Ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam.

“Huu ni mpango wa Taifa uliowekwa wazi ndani ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kuhakikisha nchi inakuwa na uhuru wa kuzalisha dawa zake yenyewe,” amesema Waziri Mchengerwa.

Waziri Mchengerwa amesema Taifa limejipanga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, kiwango cha uzalishaji wa dawa kuongezeka kutoka asilimia 10 ya sasa hadi kufikia asilimia 65.

“Mpango huu ni mpango wa Taifa unaoongozwa na Rais, ili ifikapo 2030, baada ya Rais kustaafu, tuwe tumejitosheleza na tumepanda kutoka asilimia 10 hadi kufikia asilimia 65 ya uzalishaji wa dawa nchini,” amesema Waziri Mchengerwa.

"Hivi sasa tumepata wadau wa uwekezaji zaidi ya 40 kutoka mataifa mbalimbali, ikiwemo Ujerumani, Uingereza, Marekani na India, ambao watahakikisha changamoto zote zilizokumba sekta ya uzalishaji wa dawa zinatatuliwa kwa sababu wamejipanga vizuri" amefafanua Mchengerwa.

Aidha, Waziri Mchengerwa amesema kuwa kwa mipango hiyo ya Wizara ya Afya, Taifa litapiga hatua katika uzalishaji wa dawa ndani ya nchi, jambo litakalo okoa fedha za Serikali zinazotumika kuagiza dawa nje ya nchi na pia kurahisisha upatikanaji wa dawa kwa wananchi.