TUWE NA IMANI NA TIMU YA UOKOAJI, TUACHANE NA UPOTOSHAJI
Posted on: November 17th, 2024Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, ametoa wito kwa wananchi kuacha kusikiliza taarifa za upotoshaji zinazozagaa na badala yake kuwa na imani na juhudi za jeshi letu na timu ya uokoaji inayoongozwa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Dkt. Mollel, ambaye aliingia hadi ndani kwenye vyumba vya eneo la tukio ili kujionea hali halisi, amepongeza juhudi za timu hii ya uokoaji, ambayo pia ilishiriki kwa mafanikio katika zoezi la kukabiliana na janga la Hanang. Timu hiyo sasa inafanya kazi kwa umakini mkubwa kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama chini ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, kuhakikisha majeruhi wanapata msaada bila kuongeza hatari ya kuanguka kwa vifusi zaidi.
Akizungumza katika eneo la tukio la kuporomoka kwa ghorofa Kariakoo, Dar es Salaam, Dkt. Mollel amesisitiza kwamba Jeshi letu na timu ya uokoaji kinafanya kazi kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha majeruhi wanapata msaada bila kuongeza hatari ya kuanguka kwa vifusi zaidi.
“Kazi inayoendelea hapa imefanywa kwa umakini wa hali ya juu na Jeshi letu na timu ya uokoaji, kuhakikisha watu walioko ndani ya vyumba vya majengo jirani hawafunikwi na vifusi. Mimi binafsi nimeingia katika baadhi ya vyumba vya majengo ya jirani ambayo yamekuwa njia ya kuingia kwenye jengo lililoanguka,” amesema Dkt. Mollel.
Aidha, Naibu Waziri ameeleza kuwa majeruhi walioko ndani ya vyumba hivyo wamewekewa gesi ya oksijeni ili kuwasaidia kuendelea kupumua vizuri, hatua iliyowezekana kutokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya.
“Tusisahau kwamba Rais wetu amejenga viwanda vya kuzalisha oksijeni kwenye hospitali zetu, na sasa hatuna upungufu wa gesi hiyo muhimu. Hii imekuwa msaada mkubwa katika juhudi za kuokoa maisha,” amesema Dkt.Mollel.
Aidha, Ameongeza kuwa umahiri na uangalifu wa vikosi vya uokoaji umewezesha majeruhi wengi kufikishwa hospitalini wakiwa na majeraha madogo au bila majeraha makubwa, na hali zao zinaendelea kuimarika.