Ministry of Health

TANZANIA YAJITANGAZA KIMATAIFA KWA UBORA WA HUDUMA ZA AFYA, YATAJA UWEKEZAJI KATIKA MIUNDOMBINU

Posted on: August 21st, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF – Addis Ababa

Tanzania imeendelea kujijengea uwezo wa kutoa huduma bora za afya kwa kuwekeza katika miundombinu ya afya, upatikanaji wa bidhaa za afya pamoja na kuimarisha wataalamu wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, hatua ambayo imechangia kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa kutoka nje ya Tanzania.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia masuala ya Dawa na Vifaa Tiba Bw. Emmanuel Tayari, amesema hayo leo Agosti 21, 2026 pembezoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa 13 wa Kikanda wa Wadau wa Afya wa Afrika Mashariki unaofanyika Addis Ababa, Ethiopia.

“Uwekezaji huu umeanza kuleta matokeo makubwa, Idadi ya wagonjwa kutoka nje ya nchi wanaofika Tanzania kwa ajili ya matibabu imeongezeka kutoka elfu 5,705 mwaka 2022 hadi elfu 12,180 mwaka 2025,” amesema Bw. Tayari.

Aidha, Bw. Tayari amesema Tanzania imeendelea kuwekeza katika kuongeza na kuimarisha wataalamu wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, akisisitiza kuwa uwekezaji katika wataalamu wa afya ni sehemu muhimu ya kuhakikisha wananchi na wagonjwa kutoka nje ya nchi wanapata huduma bora, salama na zenye ufanisi.

Pia, Bw. Tayari amesisitiza umuhimu wa kuunganisha ufadhili wa huduma za afya na ubora wa huduma, akieleza kuwa rasilimali zinazotengwa katika sekta ya afya zinapaswa kuleta matokeo yanayopimika na kuchochea utoaji wa huduma za Afya zenye ubora zaidi.

Katika suala la udhibiti, Bw. Tayari amesema nchi za Afrika Mashariki zinapaswa kuimarisha ushirikiano na kuwa na mifumo inayofanana katika kuweka na kutekeleza viwango vya ubora wa huduma za afya, kwa kuwa changamoto ya ubora katika nchi moja inaweza kuathiri nchi nyingine kutokana na mwingiliano wa watu.

“Kwa mfano, dawa inaweza kukataliwa katika nchi moja kwa sababu haikidhi viwango, lakini baadaye ikaingia katika nchi nyingine, Hivyo, nchi za Afrika Mashariki zinapaswa kulindana dhidi ya bidhaa na huduma zisizo na ubora,” amesema Bw. Tayari.