Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TANZANIA KUANZISHA TAASISI YA TAIFA YA AFYA YA JAMII

Posted on: October 3rd, 2023


Na. WAF - Dar es Salaam


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinakusudia kuanzisha Taasisi ya Taifa ya Afya ya Jamii ili ziweze kuimarisha uwezo wa nchi zetu katika kukabiliana na kudhibiti Magonjwa ya Milipuko pamoja na Majanga. 


Waziri Ummy ameyasema hayo leo Octoba 3,2023 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 10 wa Tanzania Health Summit uliofunguliwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.  


“Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwako kupitia Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassoro Ahmed Mazrui tumesema ni wakati sasa umefika tuanzishe Taasisi za Taifa za Afya ya Jamii ili nchi zetu ziweze kuratibu uwezo wa kukabiliana na kudhibiti Magonjwa ya Milipuko pamoja na Majanga”. Amesema Waziri Ummy 


Amesema, Serikali kupitia Wizara zs Afya zitaendelea kushirikiana na wadau, mashirika yasiyo ya Kiserikali katika kuimarisha huduma za Afya nchini. 


Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali imeamua kuja na Mpango Mmoja na jumuishi wa Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii (Coordinated and Integrated Community Health Workers Programme) ili kuimarisha huduma za Afya ngazi ya msingi ambapo Wizara imeshatengeneza mtaala ambao watapatiwa mafunzo ya miezi Sita ili waweze kutoa huduma bora za Afya kwa wananchi. 


Aidha, Waziri Ummy amebainisha kuwa wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii wamekuwa wakisaidia kuibua wagonjwa wa Kifua Kikuu pamoja na kushuhulikia masuala mbalimbali ya mama na mtoto. 


Sambamba na hilo, Waziri Ummy amesema ili kufikia lengo la huduma za Afya kwa wote ni lazima kuzingatia ubora wa huduma, ugharamiaji wa huduma za Afya kupitia Bima ya Afya kwa wote pamoja na kuimarisha huduma za kinga. 


“Bado Serikali tunayo dhamira ya dhati ya kuendelea na mchakato wa muswada wa Bima ya Afya kwa wote ili kuwarahisishia Watanzania kupata huduma kwa haraka na bila kikwazo cha fedha”. Amesema Waziri Ummy