JKC, KKKT KWENYE ZAMA MPYA ZA HUDUMA ZA MOYO KANDA YA KASKAZINI ARUSHA
Posted on: January 28th, 2026Na WAF, Arusha
Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali inatekeleza mkakati wa kusogeza huduma za kibingwa na kibingwa bobezi za matibabu ya moyo karibu na wananchi ili kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza na kuboresha huduma za afya nchini.
Waziri Mchengerwa amesema hayo Januari 27, 2026 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) iliyopo Selian, mkoani Arusha.
"Hatua hii inatekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya katika ngazi zote" amesema Waziri Mchengerwa.
Waziri huyo ameipongeza JKCI chini ya uongozi wa Dkt. Kisenge kwa kusogeza huduma za matibabu ya moyo Kanda ya Kaskazini, akisema mkoa wa Arusha una umuhimu mkubwa kutokana na kuwa kitovu cha utalii na shughuli za kiuchumi.
Akizungumzia kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, Waziri Mchengerwa amesema magonjwa ya moyo yanachangia zaidi ya asilimia 32 ya vifo duniani, huku mkoa wa Arusha ukiwa miongoni mwa mikoa yenye idadi kubwa ya wagonjwa.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amewahimiza wananchi kujiunga na mpango wa bima ya afya kwa wote unaotarajiwa kuanza hivi karibuni, akisema bima ya afya inalinda familia dhidi ya gharama kubwa za matibabu na kusaidia kufanikisha lengo la afya kwa wote.
Akizungumzia maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027, Waziri Mchangerwa amesema Serikali inaunga mkono uanzishwaji wa Sports Cardiology Centre katika Hospitali ya ALMC ili kutoa huduma maalum za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wanamichezo watakaoshiriki mashindano hayo.
Aidha, Waziri huyo amesema JKCI na ALMC wameboresha huduma za dharura, kliniki za wagonjwa wa nje na wamepanga kuweka mitambo ya kisasa ikiwemo Cathlab, MRI na CT Scan, hatua itakayochochea Tiba Utalii na kuongeza ubora wa huduma za afya Kanda ya Kaskazini.
"Tangu kuanza kwa ushirikiano wa JKCI na ALMC mwezi Novemba mwaka jana, hospitali hiyo imetoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wagonjwa 11,051, huku wagonjwa 482, wakifanyiwa upasuaji mkubwa na mdogo 1,533 na kutoa huduma za tiba ya viungo kwa wagonjwa 1,297, amefafanua Waziri Mchengerwa
Waziri Mchengerwa yupo mkoani Arusha kwa ajili ya kukagua shughuli mbali mbali za huduma za afya mkoani humo.