Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TANZANIA YAPIGA HATUA MAFANIKIO YA AFYA YA MAMA NA MTOTO

Posted on: January 22nd, 2026

Na WAF,  Sweden


Tanzania imeiambia jumuiya ya kimataifa kuwa imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya Afya kutokana na uongozi thabiti wa Serikali ambao umefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa sambamba na utoaji wa huduma bora.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi katika mjadala wa mkutano wa viongozi wa Afrika  unaofanyika jijini Stockholm, Sweden leo Januari 22, 2026


Dkt. Samizi amesema kati ya mwaka 2015 hadi 2022 Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama kutoka vifo 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, ambapo katika kipindi hicho pia vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000, huku vifo vya watoto wachanga vikishuka kutoka 25 hadi 24 kwa kila vizazi hai 1,000.


Dkt. Samizi ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushiriki wa karibu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kusimamia utekelezaji wa ajenda ya afya ya mama na mtoto, pamoja na kuimarishwa kwa uwajibikaji wa viongozi wa mikoa katika ufuatiliaji wa huduma za afya.


“Serikali imeongeza upatikanaji wa huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga (CEmONC) kwa kujenga zaidi ya vituo vya afya 500 vinavyotoa huduma hizo, sambamba na kuboresha mfumo wa rufaa kupitia usafiri wa wagonjwa unaotolewa na madereva wa jamii chini ya mpango wa m-Mama,” amesema Dkt. Samizi.


Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amezishauri nchi rafiki na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Tanzania ili kuimarisha huduma za afya kwa kuwekeza zaidi katika huduma za kliniki za wajawazito ikiwemo matumizi ya teknolojia ya ultrasound na virutubisho vya micronutrients.


Pia amependekeza kuanzishwa kwa vitengo vya watoto wachanga (NCUs) katika hospitali zote za wilaya, utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (UHI), pamoja na kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa na vifaa tiba.


Dkt. Samizi amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa kikanda na kimataifa, hususan katika kipindi hiki cha changamoto za kisiasa na kiuchumi duniani, ili kulinda mafanikio yaliyopatikana na kuharakisha juhudi za kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga barani Afrika.