SERIKALI KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO HOSPITALI OLTURUMET MKOANI ARUSHA
Posted on: January 28th, 2026Na WAF,Arusha
Serikali imetoa ahadi kushughulikia changamoto zinazo ikabili Hospitali ya Wilaya ya Arumeru Magharibi inayohudumia wananchi zaidi ya 300,000 wa jimbo hilo.
Hayo yamesema na Waziri wa Afya Mhe.Mohamed Mchengerwa leo Januari 27,2026 wakati wa ziara yake kwenye Hospitali ya Wilaya Olturument Arumeru mkoani Arusha akiwa kwenye ziara ya kukagua miundombinu , vifaa tiba na hali ya utoaji huduma za Afya .
“serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya ili kuboresha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na rasilimali watu.”amesema Mhe.Mchengerwa
Awali akitoa taarifa ya hospitali, Mbunge wa Arumeru Magharibi Dkt.Johanes Lukumay amesema kuwa hospitali ina dawa za kutosha pamoja na vifaa muhimu vya uchunguzi kama Utral Sound na Digital X-ray ambazo zimewasaidia wananchi wa jimbo hilo na kuondokana na adha yakusafiri umbali mrefu kufuata huduma.
"Uwekezaji uliofanywa na Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umeleta matokeo chanya yanayoonekana wazi kwa wananchi wa jimbo hili kwani huduma iliyotulazimu kwenye KCMC au MountMeru sasa tunazipata hapa hapa" amesema Dkt. Lukumay na kuongeza.
“Jumla ya shilingi bilioni 9 zimetumika kununua vifaa tiba na kuwekeza katika miradi ya afya, hatua iliyoongeza ufanisi wa utoaji wa huduma hospitalini," amefafanua Lukumay
Dkt. Lukumay hakusita kumuel3zea Mhe. Waziri changamoto kadhaa zinazohitaji kushughulikiwa ikiwemo ujenzi wa barabara ya hospitali, upatikanaji wa maji ya uhakika safi na salama pamoja na ujenzi wa ujenzi wa uzio wa hospitali kwa usalama, pamoja na uwepo wa uhaba wa watumishi katika baadhi ya kada muhimu zikiwemo famasia (madawa) na physiotherapy.
“Tunaiomba serikali itusaidie kutatua changamoto hizi kwa maslah ya wananchi wetu .” Amesema Dkt.Lukumay
Akizungumza baada ya kupokea maombi hayo, Waziri Mchengerwa amesema maeneo yote yenye changamoto yanayohusu afya yatafanyiwa kazi kwa kushirikiana na wizara na taasisi husika. Ameeleza azma yake kuona wananchi wote wanajiunga na Bima ya Afya kwa Wote ili kupunguza gharama za matibabu na kuhakikisha wanapata huduma bora kwa wakati.
“Ninaahidi kuyabeba maombi yaliyowasilishwa na kuyafikisha kwa mawaziri wenye dhamana ya maji, barabara na ajira za watumishi ili changamoto hizo zipatiwe ufumbuzi wa haraka.”amesema Mhe.Mchengerwa
Mhe.Mchengerwa amehitimisha kwa kusema kuwa masuala ya maabara na viungo tayari yamechukuliwa na Wizara ya Afya na yatafanyiwa kazi kwa kushirikiana na TAMISEMI ili kuhakikisha hospitali inakuwa na huduma kamili kwa manufaa ya wananchi.