Ministry of Health

SERIKALI YASISITIZA USHIRIKIANO KATIKA KUKUZA NA KUJUMUISHA TIBA ASILI ZENYE USHAHIDI WA KISAYANSI

Posted on: August 28th, 2026

Na Andrea Kadege, WAF-Mbeya

Serikali imesisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utafiti na ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kuhakikisha tiba asili zenye usalama, ubora na ufanisi uliothibitishwa kisayansi zinajumuishwa katika mfumo rasmi wa huduma za afya nchini.

Akizungumza katika Kongamano la 5 la Kisayansi la Tiba Asili linalofanyika jijini Mbeya leo Agosti 28, 2026, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Tiba Asili Dkt. Winfrida Kidima, amesema ujumuishaji wa tiba asili katika mfumo rasmi wa afya unapaswa kwenda sambamba na ushahidi wa kisayansi, hususan katika maeneo ya usalama, ufanisi, udhibiti wa ubora wa bidhaa za dawa, matumizi sahihi ya dawa na mifumo madhubuti ya kufuatilia matokeo na madhara yanayoweza kujitokeza.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya, NIMR na wadau wengine inaendelea kuchukua hatua za kuimarisha tafiti, maabara, kuandaa miongozo ya kitaifa ya utafiti wa tiba asili pamoja na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa bidhaa za tiba asili zenye ubora.

Aidha, amesisitiza kuwa mafanikio ya ujumuishaji wa tiba asili hayawezi kufikiwa na taasisi moja pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali ukiwemo watafiti, waganga wa tiba asili, sekta binafsi, taasisi za udhibiti na watoa huduma za afya.

Amesema kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kubadilishana matokeo ya tafiti na kuibua mawazo yatakayosaidia kuongeza ushahidi wa kisayansi, kuimarisha mifumo ya udhibiti na ufuatiliaji, kujenga uwezo wa watoa huduma na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za tiba asili zenye ubora.

Aidha, amewapongeza NIMR na Kamati ya Maandalizi kwa kuandaa kongamano hilo, huku akiwataka washiriki kutumia fursa hiyo kujadili kwa kina masuala yatakayochangia kuboresha afya na ustawi wa Watanzania.

Serikali imeendelea kusisitiza matumizi ya tiba asili zilizo salama na zenye ufanisi, sambamba na usajili na udhibiti wa wataalamu na bidhaa hizo ili kulinda afya ya jamii.