Ministry of Health

TANZANIA, CHINA ZAFUNGUA UKURASA MPYA WA HUDUMA BINGWA ZA MOYO

Posted on: September 19th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam

Serikali ya Tanzania na China zimeingia makubaliano ya kusaini mkataba wa ujenzi wa jengo jipya la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika eneo la Mloganzila, Dar es Salaam wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 119.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, amesema hayo leo Septemba 19, 2026 wakati wa utiaji sain kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya watu wa China yaliyosainiwa na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian jijini Dar es Salaam.

"Tanzania na China zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu katika sekta ya afya ambapo wataalamu kutoka China wamekuwa wakishirikiana na wataalamu wa Tanzania katika maeneo mbalimbali, ikiwemo magonjwa ya moyo na huduma nyingine za kibingwa," amesema Dkt. Magembe

Aidha, Dkt. Magembe amesema ushirikiano kati ya Tanzania na China umewezesha kuimarika kwa JKCI ambayo kwa sasa haitoi huduma kwa Watanzania pekee, bali pia wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, Ukanda wa Maziwa Makuu na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Amesema, ongezeko la mahitaji ya huduma za moyo limeifanya Serikali kuendelea kupanua uwezo wa JKCI, ikiwemo ujenzi wa jengo jipya Mloganzila, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Magembe amesema Tanzania imechaguliwa kuwa miongoni mwa vituo vya umahiri vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika maeneo matatu ambayo ni magonjwa ya moyo, upandikizaji wa viungo pamoja na afya ya kinywa na meno.

Dkt. Magembe amesema ushirikiano wa Tanzania na China katika afya umeendelea kupanuka na sasa unahusisha pia masuala ya Usalama wa Afya Duniani, ikiwemo kuimarisha maandalizi na mwitikio wa milipuko ya magonjwa na vitisho vingine vya afya.

Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian, amesema JKCI ni mfano wa matokeo ya ushirikiano wa Tanzania na China, akieleza kuwa China imeendelea kusaidia upanuzi wa taasisi hiyo, ikiwemo ujenzi wa jengo jipya lenye vitanda 100, maabara za utafiti na ofisi za utawala.