UNGA 2026: TANZANIA YAIHAKIKISHIA DUNIA UZALISHAJI WA DAWA NA KUBORESHA AFYA AFRIKA
Posted on: September 22nd, 2026Na John Mapepele, WAF-New York
WAZIRI wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Tanzania itaendelea kuweka kipaumbele katika kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa, bidhaa za afya na vifaa tiba, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje, kuimarisha usalama wa afya nchini na barani Afrika kwa ujumla.
Mhe. Mchengerwa amebainisha hayo leo, jijini New York, Marekani, wakati akizungumza katika kikao cha ‘Sustaining Sierra Leone’s Triple Zero Gains Through 2028’, ambapo ameiwakilisha Tanzania akiambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Grace Magembe katika mjadala kuhusu namna ya kudumisha mafanikio yaliyopatikana Sierra Leone katika kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kuongeza huduma za chanjo.
Kikao hiki ambacho kimeratibiwa na Serikali ya Sierra Leone kinafanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) katika kikao cha 81 (UNGA 81), unaowakutanisha wawakilishi wa nchi zote 193 wanachama wa UN na kila nchi ina kura moja ambapo kwa Tanzania, Makamo wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi anamwakilisha Rais, Mhe Rais Samia Suluhu kuongoza ujumbe wa Tanzania.
Akizungumza katika mkutano huo Mhe.Mchengerwa amefafanua kuwa Tanzania inaunga mkono kikamilifu Mpango wa Umoja wa Afrika wa AU Champion Roadmap 2026–2030 unaolenga kufikia malengo ‘zero tatu’, ambayo ni kutokuwepo kwa uzazi wa nyumbani na usio na wataalamu, kutokuwepo kwa vifo vya mama na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika, pamoja na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo.
“Tanzania inajivunia kuwa na Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika katika ajenda hii. Chini ya uongozi wake, tunaunga mkono kikamilifu AU Champion Roadmap 2026–2030 na Zero tatu,” amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha huduma za afya zinapatikana jirani na wananchi wote nchi nzima pia Serikali inaimarisha mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote na kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za afya ya mama na mtoto na kuwalinda wananchi dhidi ya gharama kubwa za matibabu.