Ministry of Health

AMBULANCE KULETA AHUENI HUDUMA ZA DHARURA NYARUYОBA

Posted on: September 17th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Kibondo


Wananchi wa Nyaruyoba na maeneo jirani wamepata ahueni baada ya Kituo cha Afya Nyaruyoba kukabidhiwa gari la wagonjwa (ambulance), litakalosaidia kurahisisha usafirishaji wa wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura na rufaa.


Ambulance hiyo imekabidhiwa leo, Septemba 17, 2026, na Naibu Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, Dkt. Florence Samizi, katika Kituo cha Afya Nyaruyoba, Kata ya Nyaruyoba, Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Mkoa wa Kigoma.


Dkt. Samizi ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kutenga fedha za mafuta ili gari hilo liwe tayari wakati wote na liweze kuwafikisha wagonjwa katika vituo vyenye huduma za juu bila kuchelewa.


Amesisitiza pia kuwa wagonjwa wanaotumia ambulance hiyo hawapaswi kutozwa gharama za mafuta, akiwataka viongozi na watumishi wa afya kuhakikisha huduma hiyo inatumika kwa wagonjwa wenye uhitaji na kwa malengo yaliyokusudiwa.


Kwa mujibu wa Dkt. Samizi, uwepo wa ambulance hiyo utaongeza uwezo wa Kituo cha Afya Nyaruyoba kutoa huduma za rufaa, hasa kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ambayo hayapatikani katika kituo hicho.


Amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu na mazingira ya utoaji wa huduma, hatua inayolenga kuwafikishia wananchi huduma muhimu kwa wakati na karibu na maeneo wanayoishi.


Dkt. Samizi ameitaka Halmashauri na watumishi wa afya kulitunza ambulance hiyo na kuhakikisha inapatikana wakati wa dharura, ili iwe msaada wa kudumu kwa wananchi wa Nyaruyoba na maeneo yanayozunguka kituo hicho.