TANZANIA YAJIANDAA KWA MKUTANO WA 26 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA AFYA EAC
Posted on: September 23rd, 2026Na WAF– Dodoma
Wizara ya Afya imefanya kikao cha maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 1 hadi 6 Oktoba 2026.
Kikao hicho kimefanyika leo, Septemba 23, 2026, katika ukumbi wa Public Health Emergency Operations Centre (PHEOC), Mtumba, Dodoma, na kuwakutanisha wataalamu na wadau mbalimbali kutoka Wizara ya Afya Tanzania Bara na Zanzibar, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, TMDA, MSD, BMH, NIMR, Wizara ya Elimu pamoja na Chuo Kikuu cha Muhimbili.
Akizungumza katika kikao hicho, Mratibu wa EAC na Afrika CDC, Dkt. Michael Kiremeji, amesema maandalizi hayo yanalenga kuhakikisha Tanzania inakuwa na uratibu mzuri katika kushiriki mkutano huo na kuchangia katika mijadala ya masuala ya afya yanayolenga kuimarisha ustawi wa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesema mkutano huo pia utatoa fursa ya kujadili utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa katika mikutano iliyopita, pamoja na maendeleo ya programu na miradi mbalimbali ya afya inayotekelezwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amebainisha kuwa,lengo la kikao hicho ni kuweka uratibu wa pamoja na maandalizi ya Tanzania kuelekea mkutano huo, ikiwemo kupitia ajenda mbalimbali zitakazojadiliwa pamoja na kuhakikisha Tanzania inashiriki kikamilifu katika mijadala na maamuzi yatakayofanyika.
“Kikao hiki cha maandalizi kinalenga kuhakikisha maandalizi ya Tanzania yanakuwa na uratibu mzuri na kuwezesha majadiliano kuhusu utekelezaji wa maamuzi ya mikutano iliyopita pamoja na programu na miradi mbalimbali ya afya katika Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema Dkt. Kiremeji.
Dkt.Kiremejj amesisitiza kuwa,Mkutano huo wa EAC utafanyika katika ngazi tatu, ambapo kuanzia tarehe 1 hadi 4 Oktoba 2026 kutakuwa na kikao cha wataalamu, tarehe 5 Oktoba 2026 kitafanyika kikao cha Makatibu Wakuu, huku tarehe 6 Oktoba 2026 kikifanyika kikao cha Mawaziri wa Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.