Ministry of Health

SERIKALI YAIMARISHA TIBA ASILI, WATOA HUDUMA 71,183 WASAJILIWA

Posted on: August 31st, 2026

Serikali imesema inaendelea kuimarisha na kurasimisha sekta ya Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini, huku ikisisitiza umuhimu wa wananchi kupata huduma kutoka kwa watoa huduma na vituo vilivyosajiliwa.

Akitoa Salaam za Mganga Mkuu wa Serikali kwenye kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika yanayofanyika Viwanja vya Uhindini, jijini Mbeya, Dkt. Goodlove Mbwanji, Mkurugenzi wa Hospitali ya Kanda Mbeya, amesema kuwa Tiba Asili imekuwa sehemu ya maisha ya Watanzania kwa muda mrefu na inakadiriwa kunufaisha zaidi ya asilimia 60 ya wananchi.

"Katika mwaka wa fedha 2025/26 jumla ya watoa huduma na wataalamu 9,156 walisajiliwa, na kufanya idadi ya waliosajiliwa kufikia 71,183. Aidha, vituo vipya 258 vilisajiliwa na kufikisha jumla ya vituo vilivyosajiliwa nchini kuwa 2,304," amesema Dkt. Mbwanji.

Dkt. Mbwanji amesema Serikali pia imesajili dawa za asili 55 katika mwaka huo, na kufanya jumla ya dawa zilizosajiliwa tangu mwaka 2017 kufikia 196.

Dkt. Mbwanji ametumia fursa hiyo kuhusu umuhimu wa kuhakikisha dawa za asili zinachunguzwa na kuthibitishwa kabla ya matumizi huku amifafanua kwamba, Ufuatiliaji wa dawa zilizopo sokoni mwaka 2025 ulibaini kuwa asilimia 17 zilikuwa zimechakachuliwa, huku na asilimia 25 zikiwa na sumu kuvu.

Dkt. Mbwanji amewahimiza wananchi kuwa makini na dawa zisizo na usajili na kuhakikisha wanapata huduma kutoka kwa watoa huduma na vituo vilivyosajiliwa.

Katika hatua nyingine, Serikali imeendelea kuunganisha Tiba Asili na huduma za kisasa za afya. Dawa 45 za asili ziliingizwa katika huduma jumuishi kuanzia mwaka 2023, na huduma hizo sasa zinapatikana katika hospitali 14 za Rufaa za Mikoa.

"Kufikia Januari 2026, jumla ya wagonjwa 2,300 walikuwa wamepatiwa huduma za Tiba Asili kupitia hospitali hizo.

Serikali imefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2026/27, inaendelea kujenga uwezo wa watumishi wa hospitali nyingine za rufaa na kuanza kushusha huduma hizi hadi ngazi ya Halmashauri za Wilaya ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika kwa imefanyika jijini Mbeya kuanzia Agosti 25 hadi 31, 2026.