Customer Feedback Centre

Ministry of Health

RAIS WA COMORO ASIFU USHIRIKIANO WA TANZANIA KATIKA HUDUMA ZA MATIBABU

Posted on: October 7th, 2025

Na, WAF-Anjouan, Comoro 


Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Kanali Azali Assoumani, amefanya ziara katika Kambi Maalum ya Matibabu ya Kibingwa inayofanyika katika Hospitali ya Hombo, kisiwani Anjouan. 


Ziara hiyo ya kihistoria imefanyika kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango wa madaktari bingwa kutoka Tanzania ambao wamekuwa wakitoa huduma za bure kwa wananchi wa Comoro, hususan katika kisiwa cha Anjouan.


Katika ziara hiyo, Rais Azali ameambatana na viongozi waandamizi wa Serikali akiwemo Gavana wa Kisiwa cha Anjouan, Dkt Zaidou Youssouf, Waziri wa Afya wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Ahamadi Sidi Nahouda na Waziri wa Ulinzi, ambaye pia ni Katibu wa Rais na Katibu Mkuu wa Chama Tawala cha CRC, Mhe. Youssoufa Mohamed Ali.


Rais Azali amepata fursa ya kuzungumza na madaktari hao 52, na kutoa shukurani kwa namna walivyotoa huduma kwa moyo wa kujitolea, huku akielezea furaha yake kwa uhusiano mzuri kati ya Comoro na Tanzania.


“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa moyo wake wa kindugu na wa kibinadamu. Huduma hii si ya kirafiki tu bali ni ishara ya undugu wa kweli kati ya Comoro na Tanzania. Tumeguswa sana na upendo huu wa dhati,” amesema Rais Azali


Katika ziara hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Comoro amewakabidhi rasmi kwa Rais Azali timu ya madaktari bingwa kutoka Tanzania waliotoka katika hospitali kuu tano (5) za taifa ambazo ni Muhimbili National Hospital(MNH), Benjamin Mkapa Hospital(BMH), Jakaya Kikwete Cardiac Institute(JKCI), Ocean Road Cancer Institute na Muhimbili Orthopaedic Institute(MOI)


Pia, Bohari ya Dawa (MSD) na Global Medicare ambayo ndiyo Mratibu Mkuu wa kambi hiyo zimeshiriki kikamilifu katika uratibu na uendeshaji wa kambi hiyo ya matibabu.


Katika ishara ya urafiki na mshikamano, taasisi zote saba zimetoa zawadi za upendo na kumbukumbu kwa Serikali ya Visiwa vya Comoro mbele ya Rais Azali, kama ishara ya udugu na ushirikiano wa kudumu katika sekta ya afya kati ya Tanzania na Comoro.


Kambi hiyo ya kibingwa imeendelea kuwahudumia mamia ya wananchi wa Comoro kwa huduma mbalimbali za matibabu ya moyo, saratani, mifupa, upasuaji wa kitaalam na huduma za dawa, ikiwa ni sehemu ya diplomasia ya afya na ubinadamu inayotekelezwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya.


Ziara hiyo ya Rais Azali imeongeza nguvu mpya katika uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Comoro, na imeweka msingi imara wa ushirikiano wa afya unaoendelea kuwanufaisha wananchi wa pande zote mbili.