"JIONGEZE 360 BONANZA" YAENDELEA KUIMARISHA ELIMU YA AFYA YA UZAZI KWA VIJANA-SINGIDA
Posted on: August 28th, 2026Na Zakayo Mosha-WAF SINGIDA
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la "ACTION AGAINST HUNGER" kupitia Idara ya huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto programu ya Afya ya uzazi kwa vijana limeendelea na zoezi la kuelimisha jamii hususani Vijana kwa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi Mkoani Singida kupitia njia ya bonanza ujulikanao kama Jiongeze 360 Bonanza.
Akizungumza leo Agosti 28, 2026 Wilayani ya Itigi(kata ya Mitundu) Mkoani Singida, Bw. Joachim Masunga kutoka Wizara ya Afya amesema malengo ya Jiongeze 360 Bonanza kufanyika Wilayani humo ni kuwaelimisha Vijana kuhusu masuala ya uzazi na kutambua umuhimu wa Lishe Bora.
Amesema Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na Wadau wa nje na ndani katika kuelimisha jamii ya Watanzania hususani Vijana kutambua umuhimu wa Lishe,kupinga ukatili pamoja na mambo yote yanayohusu Afya ya uzazi.
"Kwa niaba ya Wizara ya Afya kupitia Idara ya Afya ya uzazi mama na mtoto tunashukuru Shirika la "ACTION AGAINST HUNGER" kwa jinsi linavyoshirikiana nasi katika kufanikisha mpango huu muhimu wa kuelimisha vijana masuala ya Afya ya uzazi,kupinga ukatili pamoja na umuhimu wa lishe"amesema na kuongeza Bw. Masunga.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Itigi Dkt.Emmanuel Mallange ambaye pia alimwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Jesca Lebba,ameishukuru Wizara ya Afya kwa kufanikisha zoezi hilo kufanyika katika Mkoa wa Singida hususani Halmashauri ya Wilaya ya Itigi-Mitundu.
Amesema pamoja na elimu ya Afya ya uzazi kutolewa na Wataalam wa Afya katika Vituo vyote vya kutolea huduma bado uhitaji ni mkubwa kwa kundi la vijana,ametoa wito kwa Wazazi na Walezi kuwaruhusu Vijana wa kike na kiume kushiriki katika mpango wa kuelimisha vijana kupitia programu ya Jiongeze 360 Bonanza.
Mwakilishi wa Shirika la "ACTION AGAINST HUNGER" Bi. Frida Musilimu amesema Shirika Hilo litaendelea kuunga mkono Juhudi za Wizara ya Afya za kutoa elimu kwa Vijana wa kitanzania katika maeneo mbalimbali ili kukabiliana na masuala ya kupinga ukatili ,uboreshaji wa Lishe Bora na Afya ya uzazi kwa jamii.