HUDUMA ZA MADAKTARI BINGWA WA SAMIA ZAWA NEEMA KWA WANANCHI WA SINGIDA
Posted on: October 6th, 2025
Zaidi ya wananchi 6,300 mkoani Singida wamenufaika na huduma za afya za kibingwa kupitia mpango wa huduma za mkoba za madaktari bingwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2024.
Akizungumza Oktoba 6, 2025 wakati wa mapokezi ya Madaktari bingwa kwa awamu ya nne mkoani humo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Bi. Fatma Mganga, amesema huduma hizo zimekuwa mkombozi kwa wananchi wa kipato cha chini, hususan katika maeneo ya vijijini.
“Kwa kupitia huduma hizi, wananchi wengi wameweza kupata matibabu ya kibingwa bila kutumia gharama kubwa za usafiri kwenda Dodoma au Dar es Salaam. Hii ni neema kubwa iliyoletwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Bi. Mganga.
Huduma hizo zimekuwa zikitolewa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza Mei, 2024 ilihudumia wagonjwa 1,771; awamu ya pili Septemba 2024 wagonjwa 2,262; na awamu ya tatu Mei, 2025 wagonjwa 2,279 kufikisha jumla ya wagonjwa 6,312 waliopatiwa huduma za kibingwa.
Bi. Mganga amezitaka Halmashauri zote kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji huduma, ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba, dawa na vitendanishi, sambamba na kuhamasisha wananchi kujitokeza kupata huduma hizo wanapofika madaktari bingwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Madaktari Bingwa wa Samia mkoani Singida, Bi. Notgera Ngaponda, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na huduma za kibingwa, hata katika vituo vya afya vya ngazi ya msingi.
Mkoa wa Singida kwa sasa una madaktari bingwa 32 na wauguzi bingwa wawili (2) waliopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, na ujio wa madaktari bingwa wa Rais Dkt. Samia umeongeza ufanisi wa huduma, ukileta matumaini mapya kwa wananchi wengi zaidi.