Ministry of Health

BIMA YA AFYA NI MSINGI WA HUDUMA BORA ZA AFYA KWA WOTE

Posted on: July 25th, 2026

Na Andrea Kadege, WAF-Arusha

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, ameendelea kuweka msisitizo kwa wananchi kuendelea kujiunga na bima ya afya, akieleza kuwa ndiyo msingi endelevu wa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya bila kujali uwezo wake wa kifedha.

Dkt. Magembe amesema hayo leo Julai 25, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Arusha, Mount Meru, alipokagua utoaji wa huduma za afya na kuzungumza na Madaktari Bingwa na Bobezi wanaoshiriki kambi ya huduma za kibingwa ya upasuaji iliyoratibiwa na ECSA HC na wadau wengine inayoendelea hospitalini hapo.

Amesema huduma za afya zina gharama duniani kote, hivyo si rahisi kwa mwananchi kutegemea kulipia matibabu kutoka mfukoni kila anapougua, "Kama wananchi anaweza akakatia bima ya gari, pikipiki, na nyumba, lazima pia tumuelimishe aone umuhimu wa kukatia bima afya kwa kuwa afya ndiyo msingi wa maisha na shughuli zote za uzalishaji.

"Afya ikiyumba huwezi kufanya kazi, huwezi kuendesha biashara wala kutunza familia, ndiyo maana ni muhimu kila mwananchi kuona thamani ya kuwa na bima ya afya ili apate huduma kwa wakati anapohitaji," amesema Dkt. Magembe.

Dkt. Magembe amesema bima ya afya ndiyo msingi wa kufanikisha huduma za afya kwa wote (Universal Health Coverage), kwa kuwa inaongeza upatikanaji wa huduma, uwezo wa wananchi kugharamia matibabu na ubora wa huduma zinazotolewa.

Amefafanua kuwa dhana ya bima ya afya ni kuchangiana, ambapo michango ya wanachama huunda mfuko unaowezesha kununua dawa, vifaa tiba na mahitaji mengine muhimu, ili mgonjwa anayehitaji matibabu apate huduma bila kuchelewa hata kama gharama za matibabu ni kubwa.

Aidha, amewataka wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya, huku akipongeza uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali katika sekta ya afya chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema umeimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na bobezi nchini, kuongeza vifaa tiba na kupunguza ulazima wa wananchi kufuata huduma hizo nje ya nchi.