Customer Feedback Centre

Ministry of Health

BILIONI NNE KUANZA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA UKEREWE

Posted on: March 13th, 2024



Na. WAF - Mwanza

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya imetenga Tsh: Bilioni Nne katika bajeti ya Mwaka huu 2023/24 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Ukerewe Mkoani Mwanza ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za Afya ikiwemo huduma za Kibingwa.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Machi 13, 2024 wakati wa ziara katika Mkoa wa Mwanza alipoambatana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Stanslaus Nyongo.

“Tunamshukuru sana Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan, tunapoelekea Miaka Mitatu ya Rais Samia kwakweli amefanya mambo makubwa sana katika Sekta ya Afya ikiwemo kutenga fedha kiasi cha Shilingi Bilioni Nne kwa ajili ya kujenga Hospitali mpya ya Rufaa ya Ukerewe ambayo itakua na huduma zote ikiwemo huduma za Kibingwa.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, fedha hizo zimepelekwa Mkoani watangaze tenda ya kupata mshauri na mkandarasi wa kujenga Hospitali hiyo ili watu wa Ukerewe wapate huduma zote za Afya karibu ikiwemo huduma za Kibingwa katoka Hospitali ya Ukerewe.

Waziri @ummymwalimu amesema kazi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaonekana kwenye dawa, vifaa tiba, kwenye watumishi pamoja na maeneo mengine mengi makubwa aliyoyafanya katika Sekta ya Afya.

Aidha, Waziri Ummy ameutaka uongozi wa Mkoa wa Mwanza kuendelea kuimarisha miundombinu ya maji taka, maji safi pamoja na kutoa elimu ili wananchi wajikinge na magonjwa ya milipuko ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu.

Pia, Waziri Ummy amesisitiza kwa Halmashauri pamoja na wadau katika Sekta ya Afya kuajiri watumishi wa Afya wa mikataba ili kuongeza idadi ya watumishi na wananchi wapate huduma bora na kwa haraka.

Mwisho, Waziri Ummy ametoa rai kwa Watanzania kuzingatia ulaji wa vyakula ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya sukari, chumvi a mafuta, kuacha tabia bwete, kufanya mazoezi ili kupunguza magonjwa Yasiyoambukiza ikiwemo Kisukari na Shinikizo la Juu la damu kwa kuwa maradhi hayo ni gharama kubwa kuyatibu.