WODI MPYA 27 ZA WATOTO WACHANGA ZAANZA KUTOA HUDUMA
Posted on: August 8th, 2024
-Matunda ya kampeni ya Madaktari bingwa wa Rais Samia
Na WAF - Dar Es Salaam
Kampeni ya Madatari Bingwa wa Rais Samia iliyofika kwenye Hospitali zote za Halmashauri 184 nchini Tanzania bara imesaidia kuanza kwa kutolewa huduma kwenye wodi maalum 27 kwa ajili ya matibabu ya watoto wachanga wagonjwa na waliozaliwa na uzito pungufu (Neo-natal Care Unit -NCU) nchini.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu Agosti 7, 2024 Jijini Dar Es Salaam wakati akitoa ripoti ya kampeni hiyo iliyoleta mafanikio makubwa kwa kusogeza huduma za Afya karibu zaidi na wananchi na pia kuongezea ujuzi wataalam kwenye Hospitali za Wilaya.
“Katika zoezi hili madaktari bingwa wameimarisha “NCU” 129 zilizokuwepo, wameanzisha mpya 27 na wamesaidia hospitali 28 kuweka mipango kazi ya kuanzisha NCU ndani ya miezi 6 ambayo ni saaa na asilimia 85." Amesema Waziri Ummy
Aidha, katika taarifa yake Waziri Ummy amebainisha kuwa kupitia Kampeni hiyo wataalam bingwa wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto waliweza kufika kwenye Hospitali za Wilaya na kutoa mafunzo elekezi kwa wataalam waliopo eneo husika na sasa wameanza kutoa huduma kwenye NCU hizo mpya.
“Haya ni mafanikio makubwa kwa Sekta ya Afya ambayo yanaifanya Tanzania kuweka rekodi chanya katika uanzishaji wa NCU, malengo ya kimataifa ni angalau kuhakikisha asilimia 80 ya Hospitali za Halmashauri zina wodi mahususi kwa ajili ya kuhudumia watoto wachanga wagonjwa (NCU) ifikapo mwaka 2025.” Amefafanua Waziri Ummy
"Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake, utashi wake na ufuatiliaji wake wa karibu uliowezesha kufikia malengo haya yanayopatikana sasa na tunaahidi Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau wa Sekta ya Afya tutaendelea kuziimarisha NCU kwa kuhakikisha zina vifaa tiba vya kutosha, kuimarisha ujuzi wa watoa huduma na kuongeza NCU nyingine katika ngazi Vituo vya Afya." Amesema Waziri Ummy