WIZARA YA AFYA YATOA ELIMU KWA WAHARIRI DHIDI YA MAGONJWA YA MLIPUKO
Posted on: October 28th, 2024Na WAF, Dar es Salaam.
Wizara ya Afya imewaasa wahariri wa vyombo vya habari kote nchini kuendelea kutumia kalamu zao na majukwaa yao ya kihabari kutoa elimu kwa jamii kuhusu kujikinga na kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko hususani ugonjwa wa Mpox, Kipindupindu na Marburg.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma Dkt. Ona Machangu Oktoba 28, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilicholenga kujadili mikakati ya ushirikiano itakayowezesha wahariri kutumia taaluma na kalamu zao kuifikisha elimu sahihi kwa jamii ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko na kwa wakati.
"Mpaka sasa Tanzania ni salama, wahariri kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tunaweza kuendelea kuikinga jamii na nchi yetu kwa ujumla dhidi ya magonjwa haya ya mlipuko, tuelimishe na kuhamasisha jamii ili iweze kuchukua hatua za kujikinga kama kunawa mikono kwa maji safi na sabuni, kuepuka kushikana mikono na njia nyinginezo za kujikinga na magonjwa haya,” amesema Dkt. Ona.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya, Bi. Roida Andusamile amesema semina ya wahariri ni sehemu ya utaratibu wa Wizara wa kukaa pamoja na wadau hao ili kuwapatia elimu muhimu itayowasaidia kutoa taarifa kwa usahihi zinazosaidia kuimarisha mapambano dhidi ya magojwa ya mlipuko.
“Tunafanya kazi kwa kushirikiana kwa sababu ni muhimu kuwa na vikao vya pamoja kwa ajili kutathimini kwa pamoja kujua nini kifanyike ili pia taarifa za Wizara ziweze kuifikia jamii," amesema Bi. Andusamile.
Bi. Andusamile amewasihi wahariri kutosita kuwasiliana na Wizara wanapotaka ufafanuzi wa jambo lolote linalohusu masuala ya afya kwani milango ya wizara ipo wazi, hivyo watapewa ushirikiano wakati wote.
Akizungumza kwa naiaba ya Wahariri, Mhariri Gazeti la Nipashe Bi. Salome Kitomari amesema kwa kuzingatia wajibu wa msingi wa vyombo vya habari, wahariri baada kupatiwa uelewa watakwenda kwenye jamii wakiwa na taaluma yenye mashiko.