WIZARA YA AFYA YAENDELEA KUIMARISHA UTAYARI WATUMISHI KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MILIPUKO TARIME
Posted on: September 3rd, 2026Na Happyness Hans, WAF - Mara
Wataalamu kutoka Wizara ya Afya kupitia Idara ya Dharura na Maafa, Kitengo cha Uhakiki wa Ubora wa Huduma wamefanya ziara katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Kituo cha Afya Mugena kwa lengo la kutathmini na kuimarisha utayari wa vituo hivyo katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko, hususan Ebola.
Ziara hiyo imefanyika leo Septemba 2, 2026, ikilenga kukagua mazingira ya vituo, mifumo ya udhibiti wa maambukizi, utunzaji wa taka pamoja na uwezo wa vituo kutoa huduma salama endapo kutatokea mlipuko wa ugonjwa.
Akizungumza, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Tarime, Dkt. Yona Charles, amesema timu kutoka Wizara ya Afya imefanya ziara hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi na kuimarisha utayari wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko.
Amesema wataalamu wamekagua usafi wa mazingira, namna taka zinavyotengwa na kushughulikiwa, pamoja na Kitengo cha Huduma za Dharura na Ajali (Emergency), huku wakitoa maelekezo ya kitaalamu kuhusu maeneo yanayohitaji maboresho ili huduma zitolewe kwa ufanisi na kwa kuzingatia viwango vya usalama.
Vile vile Dkt. Yona amesema pamoja na kukagua hospitali hiyo, timu imetembelea Kituo cha Afya Mugena ambacho kimetengwa maalum kwa ajili ya wagonjwa wa magonjwa ya milipuko, ambapo wataalamu wametoa mwongozo kuhusu namna kituo hicho kinavyopaswa kutengwa na kuandaliwa ili kiweze kutoa huduma kwa usalama.
Naye Bi. Beatrice Turuka, Muuguzi hospitali ya mji tarime amesema ziara hiyo ni muhimu katika kuimarisha maandalizi na uwezo wa vituo vya afya kukabiliana na magonjwa ya milipuko pia amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali pamoja na wataalamu wa afya katika kuboresha miundombinu, mazingira na uwezo wa watumishi, akisisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema ili kulinda afya na usalama wa wananchi.
Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mugena, Dkt. Hamza Mangosongo, amesema ziara hiyo imewasaidia kutambua maeneo yanayohitaji maboresho na kuimarisha ubora wa mazingira ya kituo, ili kuhakikisha kinakuwa tayari kupokea na kuwahudumia wagonjwa.