TANZANIA YAWAFUNGULIA 'PHILANTHROPISTS' WA UINGEREZA FURSA ZA KUWEKEZA KATIKA SEKTA YA AFYA
Posted on: August 31st, 2026Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania imewakaribisha Taasisi ya Kimataifa ya 'philanthropists' kutoka Uingereza kushirikiana katika kuimarisha mifumo ya sekta ya afya nchini kwa kuwekeza katika huduma za afya ya msingi, afya kidijitali, ubunifu na teknolojia, ufadhili endelevu pamoja na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi.
Wito huo umetolewa leo Agosti 31, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, alipokutana na ujumbe huo wa 'philanthropists' kutoka Uingereza katika ziara iliyoratibiwa na Ofisi ya Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, jijini Dar es Salaam.
"Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha viashiria vya afya katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, ikiwemo kupunguza vifo vya mama kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, mafanikio hayo yametokana na uwekezaji wa Serikali pamoja na ushirikiano na sekta binafsi, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo," amesema Dkt. Magembe
Aidha, Dkt. Magembe amesema uzoefu wa Tanzania kupitia mfumo wa 'Sector-Wide Approach (SWAp)' umeonesha umuhimu wa washirika kuelekeza rasilimali katika vipaumbele vya kitaifa na kuimarisha mifumo iliyopo, badala ya kuanzisha mifumo inayofanya kazi sambamba na Serikali.
Katika eneo la ufadhili wa afya, Dkt. Magembe amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance) kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma, uwezo wa wananchi kumudu gharama na kuboresha ubora wa huduma za afya.
Katika hatua nyingine Dkt. Magembe, ametaja maeneo yenye fursa kubwa za ushirikiano kuwa ni kuimarisha huduma za afya ya msingi, mifumo ya taarifa za afya, afya kidijitali, matumizi ya Akili Bandia (AI), pamoja na kukuza ubunifu na uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini ambapo uwekezaji katika maeneo hayo utasaidia kuimarisha ufanisi wa huduma, kupunguza mzigo kwa wahudumu wa afya na kuwezesha maamuzi yanayotegemea taarifa sahihi.