TIBA ASILI NI MUHIMU KATIKA KUBORESHA AFYA YA JAMII
Posted on: August 28th, 2026Na Andrea Kadege, WAF-Mbeya
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Prof. Said Aboud, amesema tiba asili ni eneo muhimu katika kuboresha afya ya jamii, kukuza uchumi na kuchochea maendeleo endelevu nchini.
Prof. Aboud ameyasema hayo leo Agosti 27, 2026 jijini Mbeya wakati akizungumza katika Kongamano la 5 la Kisayansi la Tiba Asili, lililoandaliwa na NIMR kwa kushirikisha wataalamu, watafiti na wadau mbalimbali katika kujadili maendeleo, ubunifu na matumizi salama ya tiba asili nchini.
"Kongamano hili la Kisayansi la Tiba Asili limeendelea kuwa jukwaa muhimu kila mwaka katika kuibua, kubadilishana na kuendeleza maarifa, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika eneo la tiba asili" amesema Prof. Aboud
Ameeleza kuwa, Tiba asili ni eneo ambalo limeendelea kuwa miongoni mwa vipaumbele vya taifa. Nchini Tanzania, kama ilivyo katika maeneo mengi barani Afrika, tiba asili imeendelea kuwa na umuhimu mkubwa katika kuboresha afya na ustawi wa jamii.
Amesisitiza kuwa kuiendeleza tiba asili, siyo tu kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za afya, bali pia tunachangia katika kukuza uchumi na maendeleo endelevu kupitia matumizi bora ya rasilimali za asili, uendelezaji wa viwanda na kuongeza ushirikiano katika utoaji wa huduma za afya zinazokidhi mahitaji ya jamii.
"Kupitia kituo chetu cha tafiti za tiba asili na tiba mbadala, Serikali imeendelea kufanya tafiti na kuimarisha ushahidi wa kisayansi kuhusu tiba asili, ili kuhakikisha matumizi yake yanafanyika kwa usalama, ufanisi na kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika" ameongeza Prof. Aboud
Amesema hatua hizi zinalenga kuhakikisha kuwa dawa na tiba zinazotokana na tiba asili zinakuwa na ubora unaokubalika, usalama na ufanisi, na hivyo kuwa na mchango katika kuboresha afya za wananchi akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha tafiti, ubunifu, uzalishaji na matumizi salama ya tiba asili nchini.