SERIKALI YASOGEZA HUDUMA ZA AFYA KARIBU ZAIDI NA WANANCHI
Posted on: September 2nd, 2026Na WAF, Dodoma
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi amesema Serikali imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia wananchi kikamilifu katika maeneo mbalimbali nchini.
Dkt. Samizi amesema hayo leo Septemba 02, 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Zena Maulid Katambo, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, kuhusu mpango mahsusi wa Serikali wa kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi kikamilifu.
Amesema Serikali kupitia Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya wa Tano (HSSP V) wa mwaka 2021–2026 imeweka mkazo katika kupanua upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wote, kupitia mamlaka za Serikali za Mitaa na ngazi mbalimbali za utoaji wa huduma.
Dkt. Samizi amesema katika kuimarisha sekta hiyo, Serikali imeongeza bajeti ya afya kutoka Shilingi trilioni 1.1 mwaka 2022/2023 hadi kufikia Shilingi trilioni 1.8 mwaka 2025/2026, hatua inayowezesha utekelezaji wa maboresho mbalimbali katika huduma za afya nchini.
Aidha, amesema idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya imeongezeka kutoka vituo 10,153 mwaka 2021/2022 hadi kufikia vituo 13,683 Machi 2026, hali ambayo imewezesha zaidi ya asilimia 85 ya Watanzania kupata huduma za matibabu ndani ya umbali wa kilomita tano kutoka maeneo wanakoishi.
Katika kuhakikisha vituo hivyo vinakuwa na wataalamu wa kutosha, Dkt. Samizi amesema Serikali imeajiri watumishi wa afya 53,633 wa kada mbalimbali katika kipindi cha mwaka 2021 hadi Machi 2026, ambapo wengi wao wamesambazwa katika vituo vya huduma za afya ya msingi.
Amesema ajira hizo zimechangia kuongezeka kwa idadi ya watumishi wa afya nchini hadi kufikia 182,430, hatua inayolenga kuimarisha uwezo wa vituo vya afya kutoa huduma kwa wananchi kwa ufanisi zaidi.
Sambamba na hilo, Dkt. Samizi amesema Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya wanazoweza kumudu, hususan makundi yenye uhitaji mkubwa.