SERIKALI YAIMARISHA MIFUMO YA USALAMA WA AFYA NCHINI
Posted on: August 31st, 2026Na Cletus Sanga, WAF – Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na CIHEB Tanzania chini ya Mradi wa Usalama wa Afya Duniani, imeendelea kuimarisha utekelezaji wa Ajenda ya Usalama wa Afya Duniani (Global Health Security Agenda – GHSA) kwa kutekeleza afua mbalimbali zinazolenga kuimarisha mifumo ya afya nchini, ikiwemo kinga na udhibiti wa maambukizi, ufuatiliaji wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa na kuongeza uwezo wa vituo kutambua, kuzuia na kukabiliana na vitisho vya afya ya jamii.
Akizungumza leo tarehe 31 Agosti 2026, Kaimu Mkuu wa Idara ya Uhakiki wa Ubora wa Huduma za Afya, Dkt. Joseph Hokororo, amesema mafunzo yaliyotolewa yamewawezesha wasimamizi wa ubora kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa kutumia nyenzo za uimarishaji ubora katika kutekeleza afua zinazohusiana na Usalama wa Afya Duniani.
Amesema mafunzo hayo yamewezesha kila hospitali kuandaa mpango kazi kulingana na vipaumbele na mahitaji yake, huku washiriki wakijengewa uwezo wa kutambua maeneo yanayohitaji maboresho, kupanga afua na kuweka viashiria vya kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mipango hiyo.
Dkt. Hokororo amesema utaratibu huo unasaidia hospitali kuwa na mipango madhubuti ya kuboresha mifumo ya utoaji huduma na kuhakikisha afua za Usalama wa Afya Duniani zinaingizwa katika mipango ya kawaida ya hospitali, jambo linalosaidia kuimarisha ubora na usalama wa huduma zinazotolewa.
Aidha, amesema kupitia usimamizi shirikishi pamoja na ufuatiliaji na uwasilishaji wa taarifa kwa njia ya mtandao, changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa mipango kazi zinaweza kubainishwa kwa wakati na hatua stahiki kuchukuliwa ili kuhakikisha afua zilizopangwa zinatekelezwa na kuleta matokeo yanayopimika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Mradi wa CIHEB Tanzania, Dkt. Siril Kullaya, amesema CIHEB Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuimarisha afua za afya, hususan uimarishaji wa mifumo ya afya, kinga na udhibiti wa maambukizi, pamoja na kuongeza uwezo wa vituo kutambua na kukabiliana na vitisho vya afya ya jamii.