Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WHO YAKABIDHI VIFAA VENYE THAMANI YA MIL. 112 KUDHIBITI MAGONJWA YA MILIPUKO KAGERA

Posted on: July 15th, 2025

Na WAF, Kagera


Shirika la Afya Duniani  (WHO)  limekabidhi vifaa vya afya vyenye thamani ya Mil. 112 ili kuimarisha tiba ya magonjwa ya mlipuko katika wilaya za  Biharamulo na Muleba  mkoani Kagera.


WHO imekabidhi vifaa hivyo kupitia Wizara ya Afya  ikiwa ni  muendelezo wa kupambana na magonjwa ya mlipuko ambayo yamekuwa mara kwa mara hususani mlipuko wa ugonjwa wa Murburg ambao hivi karibuni  ulijitokeza katika mkoa huo.


Kaimu Mkurugenzi wa Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya Dkt. Erasto Sylvanus amepokea vifaa hivyo leo Julai 15, 2025  kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe.


Dkt. Silvanus amevitaja  vifaa hivyo kuwa ni vitanda vya kisasa vya kulaza wagonjwa, machine za kufulia mashuka,stendi za kuwekea dawa, ndoo za kuhifadhi maji na kufanyia usafi katika vituo vya afya pamoja na vifaa  vya kufanya uchunguzi wa kina.


Kiongozi huyo wa Wizara ameongeza kuwa, vifaa vilivyopokelewa ni jitihada zinazoendelea kufanyika katika kurejesha hali nzuri ya kupambana na magonjwa ya mlipuko yanapotokea huku akiwataka  watumiaji wa vifaa hivyo kuvitunza ili viweze kukaa kwa muda mrefu ili  kuwasaidia wananchi.


"Ugonjwa huu umetupa  mafunzo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kutoa taarifa ya dharura  pale wanapoona ugonjwa usio wa kawaida, kuimarisha utayari, kushirikisha jamii pamoja na kuunganisha wadau katika kuudhibiti,"

amesema Dkt. Silvanus.


Amesisitiza kuwa, vifaa vilivyotolewa vitaongeza ujuzi na utendaji kazi kwa wataalam wa afya mkoani Kagera na ameishukuru WHO kwa utayari na usaidizi mzuri  katika kipindi chote ambacho nchi ya Tanzania na mkoa wa Kagera ulikumbwa na mlipuko wa ugonjwa huo.


Sambamba na hilo ametoa wito kwa halmashauri zote za mkoa wa Kagera kutenga bajeti ya ndani kwa ajili ya kukabiliana na 

magonjwa ya mlipuko yanayojitokeza kwa dharura kwakuwa  mpaka sasa tayari wamekuwa na uzoefu juu ya magonjwa mbalimbali ya mlipuko.


Naye  Mwakilishi  Mkazi wa  WHO Dkt. Galberth  Fadjo amesema kuwa  shirika hilo kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameweka jitihada kubwa na kuchukua hatua za haraka ya kudhibiti magonjwa yenye nguvu kama Murbug  yasisambae zaidi na kuhakikisha wanaopata ugonjwa   wanarudi katika hali ya kawaida  haraka bila kuleta madhara.


Amesisitiza kuwa, mlipuko wa ugonjwa wa Marburg  katika 

mkoa wa Kagera uliotokea  Wilaya ya Bukoba  mwaka 2023 na Wilaya ya Biharamulo mwaka  2025,  serikali ilipambana kuthibiti ugonjwa huo bila kuathiri shughuli nyingine na   kurejesha hali ya kawaida katika jamii huku akisema kuwa huo ni mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine zinazokabiliana na majanga.


Sambamba na hilo, amesema kuwa  WHO itaendelea kukabiliana na dharura kwa uharaka katika kupambana na magonjwa ya mlipuko  huku akitoa wito kwa mamlaka kutumia vifaa hivyo kutoa elimu ya kiutaalam kwa watakaovitumia na kuendelea kuweka mazingira mazuri ya kupambana na magonjwa ya mlipuko .


Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera  Bw. Steven Ndaki ameishukuru WHO pamoja na Wizara ya Afya kwa kuona umuhimu wa kupeleka vifaa hivyo vyenye thamani kubwa kwakuwa vitasaidia kuokoa maisha ya wananchi huku akitoa wito kwa wataalam kuvitunza vifaa hivyo kama walivyoelekezwa.


Ameongeza kuwa,  mkoa wa Kagera utaendelea kujiweka  tayari kwa ajili ya kukabiliana na dharura  zote za mlipuko kutokana na mkoa huo  kupakana na  nchi nyingi ambazo zinaongeza uhatarishi wa magonjwa ya mlipuko.