Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAZIRI UMMY ATAKA HOSPITALI YA MWALIMU NYERERE KUTOA HUDUMA ZA UBOBEZI

Posted on: February 5th, 2022

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema anataka Hospitali ya kumbukumbu ya Mwl. J.K. Nyerere kutoa huduma za ubobezi katika magonjwa ya mifupa na ajali maeneo ya kanda wa ziwa ili kupunguza rufaa na kero kwa wananchi kwenda Hospitali nyingine kutafuta huduma.

Waziri Ummy amesema hayo leo wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan katika Hospitali hiyo na kujionea huduma za afya zinavyotolewa pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali hiyo.

"Tunataka watu wa Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na mikoa ya jirani wenye matatizo ya mifupa badala ya kwenda MOI waje wapate huduma hiyo hapa". Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy ameongeza kuwa lengo la kuleta huduma hizo katika Hospitali ya Mwl. Nyerere ni kuinua mkoa wa Mara ili kumuenzi Baba wa taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Aidha, Waziri Ummy amesema ameshaelekeza Taasisi ya Mifupa ya MOI kuja katika Hospitali hiyo na kuweka tawi la taasisi hiyo na kuanza kutoa huduma za mifupa na ajali.

Ameongeza kuwa Serikali imetoa fedha nyingi ili kuboresha huduma za saratani katika Hospitali ya Bugando na mkakati uliopo ni kuifanya hospitali hiyo kujikita katika matibabu ya saratani huku Hospitali ya rufaa ya Chato itakua ni kituo cha kutoa huduma za kibingwa za  magonjwa ya Moyo ili kuipunguzia mzigo Taasisi ya Jakaya Kikwete.

Katika ziara hiyo Rais Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Afya kupitia makadirio ya maombi ya fedha za kumalizia ujenzi wa Hospitali hiyo huku Waziri Ummy akimuahidi kupeleka makadirio hayo ndani ya mwezi mmoja.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akikagua hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu J.K Nyerere, Mara.